23
Sun, Feb
12 New Articles

THBUB yafanya mazungumzo na Kaimu Jaji Mkuu

News
Typography

JUNI 8, 2017 ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ukiongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Bahame Tom Nyanduga ulitembelea Mahakama ya Rufani ya Tanzania na kufanya mazungumzo na Kaimu Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

 Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa Tume wa kukuza ushirikiano na taasisi za kitaifa katika ukuzaji wa ulinzi wa haki za binadamu na utawala bora nchini.

 Wakati wa mazungumzo mafupi baina ya ujumbe wa Tume na Kaimu Jaji Mkuu, Mhe. Nyanduga alimweleza mwenyeji wake huyo majukumu ya Tume, changamoto inazokabiliana nazo na jinsi ambavyo Tume yake inavyoweza kushirikiana na Mahakama katika ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini.

 Pia Mwenyekiti huyo alieleza mambo kadhaa ambayo Mahakama inaweza kuyashughulikia ikiwemo la msongamano wa mahabusu vituo vya polisi na magereza.

 Aidha, Mhe. Nyanduga alibainisha kuwa ufinyu wa bajeti ni moja ya changamoto kubwa inayokwamisha utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa ufanisi.

 Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu aliuhakikishia ujumbe huo kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Tume kama mdau muhimu katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu nchini.

 Aliuambia ujumbe wa Tume kwamba Mahama imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuharakisha usikilizwaji wa kesi, kupatikana hukumu, matumizi ya TEHAMA, ujenzi wa Mahakama kwa kutumia teknolojia nafuu ili kuleta ufanisi na alisisitiza suala la kupiga vita rushwa mahakamani.

 Aliongeza kuwa Tume na Mahakama zikishirikiana katika utendaji kazi zao itasaidia kuimarisha imani miongoni mwa wananchi juu ya vyombo vya utoaji haki nchini.

 Aidha, Kaimu Jaji Mkuu aliiomba Tume kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na maadili ili kujenga jamii inayochukia rushwa na kuheshimu maadili ya kazi.

 Katika ziara hiyo fupi, Mhe. Nyanduga aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Iddi Ramadhani Mapuri na Waheshimiwa Makamishna wa Tume, Dkt. Kevin Mandopi na Salma Alli Hassan.

 Wengine katika ujumbe huo walikuwa Katibu Mtendaji wa Tume, Bibi Mary Massay na Mkurugenzi wa masuala ya haki za binadamu wa Tume, Bwana Francis Nzuki.