23
Sun, Feb
12 New Articles

WADAU watakiwa kuzielewa vema changamoto zinazowakabili wazee

News
Typography

WADAU wa haki za binadamu na watanzania kwa ujumla wametakiwa kuzielewa vema changamoto zinazowakabili wazee ili kuendeleza utetezi na ulinzi wenye tija wa haki za wazee nchini.

 Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga alitoa wito huo Juni 15 mwaka huu wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa haki za wazee lililokuwa sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Mateso na Ukatili Dhidi ya Wazee Duniani. Kongamano hilo lilifanyika makao makuu ya ofisi za Tume jijini, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia.

Akiongea katika maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo: “Elewa na komesha unyanyasaji wa kipato kwa wazee; suala la haki za binadamu,” Mhe. Nyanduga alisema kuwa wazee nchini wanakabiliwa na changamoto nyingi; ikiwa ni pamoja na: unyanyapaa, kuuawa, kupigwa na kutukanwa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume changamoto nyingine zinazowakabili wazee hao ni: kutoshirikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi, lishe duni, umaskini wa kipato na magonjwa mengi.

Aidha, Mhe. Nyanduga alibainisha kuwa kumekuwepo na matukio mengi ya ubaguzi na unyanyasaji kwa wazee, hususan katika masuala yahusuyo fedha; ikiwemo mafao, kazi za muda na kupata mikopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa HelpAge International, Bw. Smart Daniel alisema kuwa wazee wengi nchini wanakabiliwa na changamoto za kiafya na kiuchumi, hivyo wanahitaji uangalizi maalumu katika jamii zetu ikiwa ni pamoja na Serikali kutenga bajeti maalumu ili kuimarisha ulinzi kwa wazee.

Idadi ya wazee duniani inaongezeka, kwa mujibu wa Bw. Daniel, takwimu zinaonyesha wapo wazee milioni 901 dunia, huku Tanzania wakiwepo wazee milioni 2.5. Na inakadiriwa ifikapo mwaka 2050 wazee duniani kote watakuwa bilioni 2.9.

Aidha Mkurugenzi huyo wa HelpAge International alisema kuwa katika kipindi cha  miaka 10 iliyopita wazee 520 wameripotiwa kuuawa nchini Tanzania, ambapo baadhi yao wakituhumiwa kwa imani za kishirikina.

Maadhimisho hayo yaliandaliwa na THBUB, kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International, yalikuwa na lengo la kujadili changamoto zinazowakabiri wazee nchini na kuweka mbinu mbalimbali za kukabiriana nazo.