23
Sun, Feb
12 New Articles

Wahitimu wa mafunzo watakiwa kuongeza ufanisi katika kazi

News
Typography


Na Getrude Alex
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),  Mhe. Dkt. Kevin Mandopi amewataka wahitimu wa mafunzo ya ufuatiliaji wa haki za binadamu na uchunguzi kutumia ujuzi walioupata ili kuongeza  ufanisi katika utendaji kazi za Tume.


Mhe. Mandopi ametoa wito huo Ijumaa, Julai 28, 2017 wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku tano kwa maafisa wa Tume.


“Bila shaka mafunzo mliyoyapata yamewaongezea uelewa zaidi katika ufuatiliaji na uandaaji wa taarifa za kiuchunguzi kuhusu masuala ya haki za binadamu, hivyo ni mategemeo ya Tume kuwa mtatumia vyema maarifa na ujuzi mlioupata kuongeza ufanisi katika utendaji kazi za Tume,” alisema Mhe. Mandopi.


Mafunzo hayo yaliyowahusisha maafisa 36, wakiwemo wakurugenzi na maafisa uchunguzi kutoka ofisi za Tume za Dar es Salaam, Zanzibar, Pemba, Lindi na Mwanza yalilenga kuwajengea  uwezo wa mbinu za kiuchunguzi na ufuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu  na biashara (Human Rights Monitoring and Investigation, Business and Human Rights).


Mafunzo hayo yaliandaliwa na THBUB kwa kushirikiana  na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika Mashariki (OHCHR -EARO -Addis Ababa) na kuwezeshwa na maafisa kutoka  OHCHR - EARO.


Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mratibu Mkazi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Bw. Alvaro Rodriguez, alisema:“Ni mategemeo yangu kuwa mafunzo haya yatawahamasisha maafisa na watumishi wa Tume kufanya kazi za kiuchunguzi kwa makini zaidi.”


Aidha, aliitaka Tume kuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kama hayo  mara kwa mara kwa maafisa wake ili kuiwezesha Tume kama taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu kutimiza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi ya kuishauri Serikali na kuwa kiungo kati ya Serikali na wadau wengine wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo,  Bw. Mitiku Mekonnen Chere, Afisa wa haki za binadamu kutoka  OHCHR -Addis Ababa aliwataka washiriki kutumia elimu waliyoipata katika kuandika  vizuri  taarifa za kiuchunguzi za masuala yahusuyo haki za binadamu.


Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo yaliyofanyika Blue Peal Hotel, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Julai 24-28, 2017 ni: ukusanyaji  wa taarifa za haki za binadamu; mbinu za kufanya mahojiano; na namna ya kumlinda mtoa taarifa, shahidi na mhanga wa tukio;uchunguzi kuhusu biashara na haki za binadamu; utetezi; na uandishi wa taarifa za kiuchunguzi.