08
Sat, Aug
3 New Articles

Tume Yahimiza Ulinzi wa Amani Nchini

News
Typography

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB), Mheshimiwa Kevin Mandopi amewakumbusha na kuwahimiza wadau wa haki za binadamu umuhimu wa kulinda amani iliyopo nchini.

 

Mheshimiwa Mandopi alitoa kauli hiyo katika mkutano wa wadau wa kupitia na kuboresha taarifa ya tathimini ya mwisho ya Mpango kazi wa haki za binadamu nchini ambao ulianza kutumika tangu mwaka 2013 hadi 2017.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Slaam Desemba 6, 2017 ulihusisha taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, Asasi za kiraia na Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) 

Akiongea wakati anahitimisha mkutano huo wa siku moja, Mheshimiwa Mandopi aliwakumbusha wadau waliohudhuria mkutano huo umuhimu wa kulinda amani katika majukumu yao ya kila siku,

“Sisi wote tunajukumu la kulinda amani ya nchi yetu, kila mtu ahakikishe analinda amani kwa kutetea vyema ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu nchini, ni lazima tuunganishe nguvu zetu kama wadau katika kulinda haki za binadamu nchini”, alisema Kamishna Mandopi

Aidha, Kamishna huyo aliwatia moyo wadau hao waliokuwa wanapitia taarifa ya tathimini hiyo ya Mpango kazi wa haki za binadamu nchini kwa kuwaambia kuwa kazi wanayoifanya inamaana kubwa kwa nchi kwani inahamasisha utetezi wa haki za binadamu.

“Nchi inapokuwa na mpango kazi wa haki za binadamu inaheshima kubwa sana kimataifa kwani inakuwa imejipambanua wazi kuwa inajali na kuthamini haki za binadamu, hivyo Tanzania kuwa na mpango kazi huu imejijengea heshima kubwa duniani”, aliongeza 

Aidha, Kamishna Mandopi alilihakikishia ushirikiano Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kufuatia kazi kubwa na msaada mkubwa unaotoa kwa Tume ili kufanikisha malengo yake ya kuhamasisha na kulinda haki za binadamu nchini.

Tathimini ya mpango kazi huo imefanywa na Washauri elekezi wawili ambao ni Bwana Yves Del Monaco na Dkt. Consolata R. Sulley.katika kipindi cha Novemba 13 hadi Desemba 8, 2017