08
Sat, Aug
3 New Articles

MASSAY aziasa AZAKI kuzingatia maadili

News
Typography

 

          Na Getrude Alex  

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Bi Mary Massay, ameziasa Asasi za Kiraia (AZAKI) kuzingatia maadili ya kitanzania wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya  kulinda, kukuza na kutetea haki za binadamu nchini.

Akifungua semina ya siku mbili ya kutiliana saini ya ushirikiano baina ya Tume na AZAKI 20, iliyofanyika makao makuu ya THBUB jijini Dar Es Salaam June 6, mwaka huu; Bibi Massay alisema kuwa, AZAKI na watetezi wa haki za binadamu kwa ujumla watakuwa na nafasi kubwa ya kufanikisha malengo yao iwapo watazingatia maadili ya kitanzania hususani matumizi ya lugha ya kistaarabu.

“Ni kitu kibaya  AZAKI kuonekana kama wapinzani au wanaharakati tufanye kazi kwa kuzingatia maadili ya kitanzania, lugha tuzizingatie kweli kweli alisema”

Kwa mujibu wa katibu mtendaji huyo, kama ilivyo kwa baba katika familia akielezwa jambo kwa heshima na anaowaongoza anasikiliza, vivyohivyo AZAKI na watetezi wa haki za binadamu wanayo nafasi kubwa ya kusikilizwa na serikali iwapo watawasilisha madai na mapendekezo yao kwa lugha ya kistaarabu.

“Tume kama chombo huru cha serikali tunaposhirikiana nanyi, tunawatarajia mzingatie sana maadili ya kitanzania” Bibi Massay alisema.

Aidha, Bibi Massay alizitaka AZAKI kutumia mamlaka zao kutoa elimu ya haki za binadamu, kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa za uvunjifu wa haki  hizo hapa nchini.

Hivyo Novemba 2017, THBUB ilizifanyia tathimini Asasi za Kiraia zipatazo 94, zinazojihusisha na masuala ya haki za binadamu nchini. Kati ya hizo AZAKI 20, 18 kutoka bara na 2 visiwani zilikidhi vigezo vya kufanya kazi na Tume na kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano.

Kwa kutambua umuhimu na nafasi za AZAKI katika kukuza, kulinda na kutetea haki za binadamu nchini, Tume imekuwa na mkakati mahususi wa kukuza mashirikiano na AZAKI hizo.

Katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini Juni 6, mwaka huu, AZAKI zinategemewa kuwasaidia wananchi ambao haki zao zimevunjwa, kuwasilisha malalamiko yao Tume au kwenye vyombo vinginevyo vilivyowekwa kisheria, kueneza elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa jamii na mtu mmojammoja, kuandaa program za pamoja za uelimishaji umma na kufanya ufuatiliaji wa uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa  misingi ya utawala bora.