14
Tue, Jul
7 New Articles

Watendaji wa Kata Waaswa Kuzingatia Haki za Binadamu Katika Maeneo Yao ya Kazi

Afisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB na Kaimu MKuu wa Kitengo cha Mipango, Bw. Laurent Burilo akitoa ufafanuzi juu ya malengo ya mafunzo kwa watendaji wa kata katika masuala ya haki za binadamu na upatikanaji wa haki kisheria, yaliyofanyika Januari 8-9, 2019, katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  (THBUB) kwa  ufadhiri wa Asasi ya Kiraia ijulikanayo kwa jina la “Legal Service Facility” (LSF), hivi karibuni imefanikiwa  kutoa mafunzo ya elimu ya haki za binadamu na upatikanaji  wa haki kisheria kwa watendaji  kata  wapatao 128 kutoka kata sita (6) za Mkoa wa  Shinyanga.

 Akieleza malengo ya  elimu hiyo kwa watendaji kata, Afisa Uchunguzi  Mkuu wa THBUB, na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mipango  Bw. Laurent Burilo amesema kuwa,  mafunzo hayo,  yalilenga kuwajengea uwezo watendaji kata juu ya masuala ya haki za binadamu, misingi ya utawala bora, kukuza  uelewa  kuhusu upatikanaji wa haki kisheria, pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya Serikali na wasaidizi wa kisheria  ili kuwawezesha watendaji kutatua migogoro mbaimbali inayowakabiri  wananchi.

Kwa upande wake  mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Wilaya  ya Kahama, Bw. Timothy Ndonya, aliwashukuru watendaji kwa kuwajibika vyema katika maeneo yao ya kazi, na  kuwapongeza kwa juhudi walizofanya katika kukomesha  mauaji ya vikongwe na albino. 

Pia aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu wanayoipata kama chachu ya mabadiriki katika maeneo yao ya kazi kwa kutenda haki  pamoja na kuhakikisha kuwa haki za binadamu hazivunjwi na wananchi wanapata huduma kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi.

“Tunategemea kuwa  watendaji kata watafikisha elimu wanayoipata kwa  watendaji wa vijiji, viongozi wa dini,  kwa wananchi, pamoja na kujenga mahusiano mazuri na wasaidizi wa kisheria” alisema Ndonya.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika wilayani Kahama Januari 8 – 9 mwaka huu, yaliwashirikisha watendaji 20, wa kata ya Kahama Mji, 18 kutoka Kata ya Msalala,  20  kutoka Halmashauri ya Ushetu, 25 kutoka kata ya Kishapu, 26 kutoka kata ya Shinyanga DC, 17  wa kata ya Shinyanga MC pamoja na wasaidizi wa kisheria  wawili (2) kutoka Shinyanga.