23
Sun, Feb
12 New Articles

THBUB, AZAKI wakutana Morogoro

Bw. Victor Rugarabamu, Mwezeshaji kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJJW), akizungumzia masuala ya mahusiano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia (AZAKI)kwenye mkutano uliofanyika tarehe 17-19 Juni, 2019, katika ukumbi wa Cherry Hotel Mjini Morogoro, uliolenga kufanyia tathimini mafanikio, changamoto na matarajio ya makubaliano hayo.

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekutana na Asasi za Kiraia (AZAKI) ilizoingia nazo makubaliano ya kushirikiana kwa lengo la   kujifunza, kubadilishana uzoefu na mawazo ya namna ambavyo taasisi hizo zitakuwa na ushirikiano wenye tija katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku.

Akifungua mkutano huo Juni 17, 2019 Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo, Alexander Hassan ambaye alimuwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora alisema kuwa 

Ni ukweli usiopingika kuwa bila mashirikiano yenye tija miongoni mwa tume  na AZAKI matokeo ya kazi zao hayatawezi kuwa makubwa.

Hivyo mkutano huo umelenga katika kuboresha ushirikiano huo ili uwe na manufaa kwa jamii wanayoihudumia.

 

“Ni wazi kuwa makundi haya mawili, yaani Tume na AZAKI yanategemeana na hivyo ni lazima tuweze kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati” alisema Hassan.

Hassan aliendelea kueleza kuwa tume inaamini katika utendaji wa pamoja, ikiwa na maana kuwa iwapo kila mdau wa haki za binadamu na utawala bora atashirikishwa kikamilifu katika ukuzaji, utetezi na ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora hatua kubwa itapigwa na ndoto ya kuwa na taifa lenye utamaduni wenye kuheshimu, kukuza na kulinda haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu itafikiwa mapema zaidi.

Aidha, Hassan alitumia nafasi hiyo kuwasisitiza AZAKI kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali. 

Mkurugenzi huyo alisema kuwa zipo baadhi ya AZAKI zinakiuka sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa – mfano, kujiingiza katika harakati za kisiasa; kuchochea uvunjifu wa amani na kubomoa umoja wa kitaifa; kukosa uaminifu na uadilifu kwa wananchi wanaofika kupata huduma kuombwa au kulazimishwa kutoa kitu kidogo ili wapewe huduma, kutumia fedha na rasilimali nyinginezo kwa matumizi binafsi au tofauti na yaliyokusudiwa. 

Aliongeza kuwa matendo kama haya yanadhoofisha harakati za ukuzaji, ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na utawala bora nchini, na kurudisha nyuma jitihada za Serikali kuleta maendeleo endelevu.

Mkutano huo uliofadhiliwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni wa siku tatu kuanzia Juni 17 hadi 19, 2019.