08
Sat, Aug
3 New Articles

Wafanyakazi Tume Wahimizwa Kuzingatia Haki na Wajibu Kazini

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Hajjat Fatuma Muya akiongea na wajumbe wa mkutano wa kumi na saba (17) wa baraza la wafanyakazi (hawapo pichani) alipokuwa akifungua mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam Januari 23, 2019. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo wa Tume, Alexander S. Hassan.

News
Typography

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Hajjat Fatuma Muya amewataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kuzingatia haki na wajibu wakati wanatekeleza majukumu yao.

 

Muya aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kumi na saba (17) wa baraza la wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora uliofanyika jijini Dar es Salaam Januari 23, 2019.

Akizungumza katika mkutano huo, Muya alisema kuwa kila mfanyakazi anapaswa kuangalia mazingira ya utekelezaji wa majukumu katika eneo lake la kazi na kushauri namna ya kuyatatua mambo yanayoathiri taasisi na utendaji kazi kwa wafanyakazi.

“Nawashauri kutimiza haki na wajibu wenu  kwa kuzingatia maadili, nidhamu na uaminifu katika utendaji kazi wenu wa kila siku na kufanya tathimini ya mwelekeo wa utendaji kazi wa taasisi”, alisema Muya

Aidha, Muya aliwakumbusha wafanyakazi hao umuhimu wa baraza la wafanyakazi kuwa ni chombo muhimu kwa ajili ya kushirikisha wafanyakazi katika kubuni, kushauri, kupendekeza na kuchangia mawazo katika uendeshaji wa utendaji kazi Serikalini.

“Mikutano hii ya baraza ndio njia bora zaidi ya kutumia vizuri uwezo na vipaji mbalimbali walivyonavyo wafanyakazi, ili kuongeza tija, ufanisi na kutoa huduma bora zaidi”, aliongeza

Mkutano huo wa kumi na saba (17) wa baraza la wafanyakazi ulilenga kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utendaji kazi wa tume na kutafuta njia bora ya kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.