08
Sat, Aug
3 New Articles

Wasaidizi wa Sheria Waelimishwa Kuwasilisha Lalamiko Kupitia Simu ya Kiganjani

Picha hapo juu ni Bw. Stanley Kalokola wakati akiwaelekeza Wasaidizi wa Kisheria namna ya kutuma malalamiko THBUB kwa kutumia njia ya ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani (SMS) wakati mafunzo yaliyofanyika Kituo cha wasaidizi wa kisheria kilichopo Momba mkoani Songwe.

News
Typography

Wasaidizi wa sheria (paralegals) waliopo Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe  wameelimishwa namna ya kuwasilisha lalamiko Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  kupitia simu ya kiganjani.

Wasaidizi hao wa kisheria wapatao kumi na mbili (12) walipata elimu hiyo katika warsha iliyoandaliwa na Tume Februari, 21-22, 2019 katika ofisi za kituo cha wasaidizi wa sheria kilichopo Momba, Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Mkoani Songwe.

Akiongea katika warsha hiyo, Muwezeshaji, Afisa Uchunguzi wa Tume, Stanley Kalokola alisema kuwa Tume imeanzisha mfumo huu wa kuwasilisha lalamiko kupitia simu ya kiganjani ili kuwarahisishia wananchi na kuwapunguzia gharama na kuokoa muda.

Kalokola aliendelea kuwaeleza wasaidizi hao kuwa mfumo huo wa mawasiliano ni kwa njia ya meseji tu na haipaswi kupiga kwani haitapokelewa.

“Mwananchi mwenye lalamiko lake au taarifa kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora anaweza kutuma ujumbe wa simu ya kiganjani kwenda namba 0737 446 787,” alisema Kalokola

Kalokola alifafanua kuwa kupitia utaratibu huo, mara baada ya lalamiko au taarifa kufika tume, Afisa wa Tume atakayelipokea anaweza kupiga simu kwa mlalamikaji ili kupata maelezo zaidi kabla ya kuanza kushughulikia lalamiko hilo.

Aidha, Kalokola aliwaeleza wasaidizi hao wa sheria kuwa ili lalamiko liweze kufika kwa usahihi, mwananchi anatakiwa kuandika lalamiko lake kwa ufupi na kulituma kwa kuanza na neno ‘REPORT’ kwenda 0737 446 787.

Mbali na kuwasilisha lalamiko kwa tume kupitia simu ya kiganjani, mlalamikaji anaweza pia kuwasilisha lalamiko lake kwa kufika katika ofisi za Tume au kuandika barua ya lalamiko lake na kuituma kwa njia ya Posta.

MWISHO.

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.