04
Tue, Aug
3 New Articles

Tume yaandaa hadidu za rejea kwa makundi ya kutetea haki za binadamu

Mratibu wa Mradi wa upatikanaji wa haki, Laurent Burilo akitoa mada kwa ufupi kuhusu mradi wa upatiakanaji wa haki katika kikao kazi cha kuandaa hadidu za rejea na muongozo kwa ajili ya makundi ya utetezi wa haki za binadamu kinachofanyika mkoani Morogoro kuanzia Juni 20-22, 2019.

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na wadau wake wanaandaa hadidu za rejea na muongozo kwa ajili ya kuyawezesha makundi ya utetezi wa haki za binadamu kufanya kazi zake vizuri.

Akifungua kikao kazi cha kuandaa hadidu za rejea na muongozo kwa ajili ya makundi hayo ya haki za binadamu kinachofanyika mkoani Morogoro kuanzia Juni 20-22, 2019,   Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka Tume, Alexander Hassan alisema kuwa hadidu za rejea na muongozo vitasaidia makundi hayo ya haki za binadamu kufanya kazi zake kwa wepesi.

 

“Hadidu za rejea zitasaidia makundi ya haki za binadamu kufanya kazi, na kwa kuwa makundi hayo yatajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya tume ni imani yangu kuwa makundi hayo yatakapoanza kazi zake yatatoa matokeo yanayotarajiwa na tume”, alisema Hassan

Katika hatua nyingine, Muwezeshaji wa kuandaa hadidu hizo za rejea, Wakili, Kaleb Gamaya alieleza washiriki wa kikao kazi hicho kuwa kazi ya kuandaa hadidu za rejea sio ndogo, inahitaji ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha zoezi hilo.

Mapema kabla kuanza kikao kazi hicho, Mratibu wa Mradi wa upatikanaji wa haki, Laurent Burilo alitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo ambao umepelekea tume kuandaa hadidu hizo za rejea.

Burilo alieleza katika kikao hicho kuwa suala la upatikanaji wa haki ni jukumu la kila mtu sio tume peke yake, kila mtu alipo ahakikishe anashirikina na tume katika uhamasishaji wa upatikanaji wa haki kwa wakati.

Makundi hayo ya kutetea haki za binadamu ni pamoja na kundi la kutetea haki za wanawake, haki za watoto, haki za wazee, haki ya Afya, haki ya kumiliki mali na haki ya kupata maji safi na salama pamoja na chakula.

Haki nyingine ni haki ya Mazingira, haki ya Elimu na haki za watu wenye ulemavu. 

Kikao kazi hicho cha siku tatu (3) kilichofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kimejumuisha wadau mbalimbali kutoka tume, Serikalini na Asasi za Kiraia.   

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.