23
Sat, Jan
1 New Articles

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Lindi, Mohamed Lihumbo (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Viongozi wa THBUB na wawakilishi wa Taasisi ya Haki Maendeleo. Wa kwanza kulia waliokaa ni Mwakilishi wa Taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba, wa pili kulia ni Kamishna wa THBUB, Amina Talib Ali. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa sheria-THBUB, Nabor Assey na Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Judica Sumari.

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wametakiwa kutatua kero zinazowakabili wananchi  katika maeneo yao ya kazi kwa wakati ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Amina Talib Ali alipokuwa akifungua mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora kwa madiwani hao yaliyotolewa na THBUB na taasisi ya Haki Maendeleo mkoani Lindi Februari 7, 2020.

Kamishna Amina aliwaeleza madiwani hao kuwa wananchi wana kero  na malalamiko mengi ambayo yanahitaji kutatuliwa na viongozi, na wao ndio viongozi waliokaribu na wananchi kuweza kutatua kero zao.

Aliendelea kuwaeleza kuwa wasiwaache wananchi wanahangaika na kero zao mpaka wakakata tamaa wakati madiwani wapo, washughulike na kero zao ili wananchi wajenge imani kwao.

“Tusiwaache wananchi mpaka wakakata tamaa na sisi, tuwashughulikie, tusikae mpaka Mhe. Rais John Magufuli aje kutatua kero hizo, rais atafanya mangapi? tusimbebeshe mzigo usio muhusu, tumechaguliwa na wananchi kuwaongoza, hivyo tuwafanyie kazi kwa lengo la kuwapa ahueni ya matatizo yao”, alisema Amina

Aliendelea kuwasisitiza madiwani hao kuwa sio kila jambo linapaswa kupelekwa Mahakamani au Polisi, bali vipo vyombo kama THBUB ambavyo kazi yake ni kusuluhisha migogoro, madiwani wawaelimisha wananchi kutumia vyombo hivyo  ili kusaidia kutatua kero zao.

“Kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya usuluhishi, serikali iliamua kuvianzisha na kuvipa mamlaka ya kuisaidia serikali kutatua migogoro mbalimbali nchini, waheshimiwa madiwani  waelimisheni wananchi katika maeneo yenu wapi pa kwenda kupata msaada pindi wanapokuwa na malalamiko yao”, alisisitiza

“Wasaidieni na waelimisheni wananchi kutambua haki zao na wajue wapi pa kwenda kupeleka malalamiko yao ili yashughulikiwe, sio kila jambo liende mahakamani, kuna mengine yanaweza kumalizwa na vyombo vya usuluhishi”, alieleza Amina

Aidha, katika hatua nyingine, Amina aliwakumbusha madiwani kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu hivyo ni muhimu kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi kwa amani.

Amina aliwahimiza madiwani  kuwaelimisha wananchi ili wajue  umuhimu wa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa, na ni muhimu kufanya hivyo kwa mustakabali mzuri wa taifa.

“Mkawahimize wananchi pia kujiepushe na vitendo visivyofaa, wazingatie sheria na taratibu zilizowekwa na serikali  na kuendelea kubaki kama raia wema na kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao bila usumbufu wowote”, aliongeza Kamishna 

 

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mohamed Likumbo aliwasisitiza madiwani kwenda kuyatumia mafunzo hayo waliyopatiwa na THBUB kwa kushirikiana na taasisi ya Haki Maendeleo kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao na kushiriki kuwasidia wananchi kutatuta migogoro mbalimbali inayowakabili.

“Katika maeneo yetu kuna migogoro ya aina mbalimbali hususani migogoro ya ardhi, tukamie ujuzi huu tulioupata leo kwenda kuwasaidia wananchi kutatua migogoro yao kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa”, alisema Meya

---Mwisho---

 

Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB akiongea katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Morogoro kuanzia Februari 3 – 4, 2020 kwa lengo la kuandaa muongozo utakaotumika kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa Magereza na maeneo mengine walipozuiliwa watu. Kulia ni Kalliopi Kambanella, Mwanasheria kutoka Dignity. Wa kwanza kushoto ni Mkurugunzi kutoka THBUB, Alexander S. Hassan, wa pili kushoto ni Una Marquards-Busk, Meneja Mradi kutoka DIGNITY na wa tatu ni Kamishna Dkt, Fatuma Rashid Khalfan.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na taasisi ya DIGNITY kutoka Denmark wamekutana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu  kuandaa muongozo wa ukaguzi na ufuatiliaji wa Magereza nchini.

Muwakilishi wa rais wa TLS, Mary Munissi (kushoto) akimkabidhi baadhi ya Machapisho ya TLS Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ametembelea Chama cha Wanasheria (TLS) jijini Dodoma na kuhimiza ushirikiano baina ya taasisi hizo.

Jaji Mwaimu alitoa kauli hiyo Januari 23, 2020 alipofanya ziara katika ofisi za chama hicho kwa lengo la kufahamiana na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano.

Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Jaji (mstaafu) Matthew Mwaimu akipokea machapisho kutoka kwa Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alipotembelea banda la kituo hicho katika maonesho ya Wiki ya Sheria viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma Februari 1, 2020. Kulia ni Afisa wa Tume, Bwana Joshua Mwambande aliyekuwa ameambatana na Mwenyekiti huyo wa Tume.

HAKIKA uongozi wa Awamu ya Nne wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora umedhamiria kukuza ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi. Hili limethibitishwa leo (Februari 1, 2020) kwa hatua ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, kutenga muda wa kutembelea mabanda ya baadhi ya wadau wake wanaoshiriki maonesho ya Wiki ya Sheria  yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Pontian Kitorobombo akiongea katika mkutano wa baraza la Wafanyakazi la THBUB

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wametakiwa kutumia vizuri mikutano ya baraza  kujadili kwa hekima  na kufanya maamuzi sahihi kwa  maslahi ya watumishi wote  ili kuleta tija kazini.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (katikati) pamoja na mwenyeji wake, Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma (watatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Sheria Februari 1, 2020 viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Wa tatu kutoka kushoto (waliosimama) ni Mhe. Jaji (Mstaafu) Matthew Mwaimu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya maadhimisho ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria yaliyoanza leo kote nchini kujua haki na wajibu wao.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja taasisi za kimataifa.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa ili serikali iweze kutimiza haki za msingi za binadamu kwa wananchi wake kikamilifu inahitaji nguvu ya kifedha ili kujenga uchumi imara utakaoweza kutimiza haki hizo.

Balozi Mahiga alitoa kauli hiyo kwenye kongamano la kitaifa la kutathimini hali ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni lililofanyika jijini Arusha Desemba 13-14, 2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI, Gilbert Sebihogo (Kushoto) akikaribishwa na mwenyeji wake Mwenyekiti wa THBUB Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu (Kulia) katika ofisi za THBUB jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa taasisi ya Haki za Binadamu Afrika (NANHRI), Gilbert Sebihogo ameishauri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kushirikiana na serikali katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi, huku akiwaasa  kujiepusha na vitendo vya kukosoa kila jambo linalofanywa na Serikali. 

Mhe. Mohamed Khamis Hamad Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), akifafanua jambo kuhusu kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu lililofanyika Ofisi za Tume Dar es salaam leo tarehe 11/12/2019.

 MAKAMU Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mohamed Khamis Hamad amewataka vijana nchini kuyaelewa malengo endelevu ya maendeleo (SDGs) ili waweze kushiriki kikamilifu kuyatekeleza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Kapt. (Mst), George Huruma Mkuchika (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Waziri huyo Mtumba, Dodoma Januari 24, 2020. Kushoto anayewatazama ni Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mohamed Hamad, na wengine katika picha ni watendaji wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Kapt. (Mst), George Huruma Mkuchika Januari 24, 2020.

Jaji Mwaimu alimtembelea  Waziri Mkuchika ofisi kwake  Mtumba, Dodoma kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kufanya kazi na kuimarisha ushirikiano baina ya ofisi hizo mbili.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika akiongea kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika kitaifa jijini Dodoma, Desemba 11, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ametoa onyo kwa watumishi wasio waadilifu na kusema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao pindi watakapobainika.

Mkuchika alitoa onyo hilo Desemba 11, 2019 kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika kitaifa jijini Dodoma.

More Articles ...

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.