23
Sun, Feb
12 New Articles

THBUB yakutana na Wadau kubuni mbinu za kuelimisha jamii

THBUB yakutana na Wadau kubuni mbinu za kuelimisha jamii

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuwashirikisha wadau wake kutoka taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia na Vyombo vya habari wamekutana katika kikao kazi cha kubuni mbinu mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu haki na haki za binadamu, hususan haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

 

Katika kikao kazi cha siku tatu kilichofanyika mkoani Morogoro kuanzia Julai 8 hadi 10, 2019 kililenga kuwashirikisha wadau katika kubuni jumbe mbalimbali za kuhamasisha, kuhifadhi na kulinda haki za makundi ya Watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.

Akiongea wakati wa kufungua kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka tume, Philipo Sungu, ambaye pia alimuwakilisha Katibu Mtendaji, alisema kuwa warsha hiyo imelenga kuandaa jumbe mbalimbali kuhusiana na maeneo ya vipaumbele na kupendekeza njia mbalimbali za kusambaza jumbe hizo.

Sungu alisema kuwa katika kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uelewa kwa umma wa sheria na haki za binadamu, hususan haki za makundi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

“Miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ya warsha hii ya siku tatu ni kuwa na jumbe mbalimbali za kutosha kwa walengwa katika kila eneo la kipaumbele  zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu haki na haki za binadamu, hususan haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu”,alisema Sungu 

“Ili kupata matokeo hayo, ninamwomba kila mmoja wenu kushiriki kikamilifu katika majadiliano kwenye vikundi na majadiliano ya pamoja na kushirikishana ujuzi na uzoefu wenu kwa moyo wote. Natambua kuwa warsha hii inawahusisha wadau wenye taaluma mbalimbali – sheria, haki za binadamu, mawasiliano ya umma, afya na elimu hivyo jopo limekamilika haswa! na nina hakika tutapata vitu vizuri” aliongeza Sungu

Kikao kazi hicho ni moja ya sehemu ya utekelezaji wa  mradi wa ‘Strengthening Access to Justice and Protection of Human Rights in Tanzania’  ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Watekelezaji wa mradi huo ni   Tume, Wizara ya Katiba na Sheria na  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Mwisho.