14
Tue, Jul
7 New Articles

Madenge: Watendaji Kata simamieni haki za binadamu.

Bi.Madenge afungua mafunzo ya Watendaji wa Kata kuhusu haki za Binadamu,yaliyofanyika katika mkoa wa Lindi Julai 8, 2019.

News
Typography

Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge amewataka Watendaji wa kata katika wilaya za Mkoa wa Lindi kusimamia haki za binadamu na upatikanaji wa haki kisheria.

Madenge alitoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa kata kuhusu haki za binadamu na upatikanaji haki kisheria yaliyofanyika katika mkoa wa Lindi Julai 8, 2019.

 

Katika mafunzo hayo, Madenge alisema watendaji wanao wajibu mkubwa wa kusimamia haki na upatikanaji haki kisheria ikiwa ni pamoja na usimamizi wa haki za watoto ambapo kwa mkoa wa Lindi kumekuwa na tatizo kubwa la mimba za utotoni kunakopelekea watoto hao kukosa haki zao za msingi. 

“Katika mkoa wa Lindi tuna tatizo kubwa la mimba za utotoni hivyo ni lazima mtambue kuwa jambo hili linasababisha watoto kukosa haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya elimu. Hivyo ni matarajio yangu kuwa mtakapo toka hapa mtakwenda kupambana na mimba za utotoni kwa kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua stahiki”, alisema  Madenge.

Madenge aliendelea kusema kuwa mkoani Lindi kuna makundi mbalimbali ambayo hushindwa kupata haki au kudai haki kisheria hasa watu wenye ulemavu kuanzia kwenye ngazi ya familia, Hivyo aliwasisitiza watendaji kwenda kutoa elimu hii kwenye maeneo wanayotoka.

Akizungumza mapema Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma na Mafunzo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Alexander S. Hassan alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yalifanyika Januari 7-11, 2019 yaliyowahusisha baadhi ya wakuu wa idara wa sekretarieti ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Lindi.

Hassan alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata kuhusu misingi ya utawala bora na haki za binadamu ili waweze kutumia elimu watakayoipata kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.  

Naye Emmanuel Lweyo, Afisa Utumishi manispaa ya Lindi ambaye ndio alikuwa Mwezeshaji wa mafunzo alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa watendaji kwani yapo mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika kutokana na kutokuwa na uelewa kwa watendaji. 

Lweyo aliongeza kwa kusema kuwa Watendaji wanapaswa kuelewa mipaka yao ya kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuweza kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Issa Mbaruku, Mtendaji wa Kata ya Kitumbikwera aliishukuru tume kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamemsaidia sana kuhusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto wa kike. 

Mbaruku aliongeza kwa kusema kuwa wao kama watendaji watakwenda kusimamia maagizo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa hasa katika kusimamia na kudhibiti mimba zo utotoni ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika katika ukatili wa kijinsia kwa Watoto.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa, Rehema Madenge aliwashukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, chini ya ufadhili wa Legal Service Facility (LSF) kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamelenga  katika kuboresha utendaji na  kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

Mafunzo hayo yamefanyika katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi ambazo ni Wilaya ya Lindi Mjini na Vijijini, wilaya ya Liwale, Wilaya ya Kilwa, Wilaya ya Ruangwa, na Nachingwea.