08
Sat, Aug
3 New Articles

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

News
Typography

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaungana na wadau wote wanaolinda na kutetea haki za watu wenye ualbino nchini kwenye kuadhimisha siku ya Kimataifa ya kutoa Elimu kuhusu dhana na haki za watu wenye ualbino duniani “International Albinism Awareness Day’’ tarehe 13/06/2018 ikiwa na kauli mbiu “KUANGAZA MWANGA WETU ULIMWENGUNI”. Kitaifa maadhimisho haya yatafanyika Mkoani Simiyu. 

Siku hii imepitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Azimio Na. A/HRC/RES/23/13 la terehe 18/12/2014. Tanzania ni mwanachama hai wa Baraza hilo, hivyo kama nchi tunapaswa kuishi tamko la Umoja wa Mataifa kwa vitendo na kutekeleza yaliyokubaliwa

Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini tunaendelea kutetea haki za watu wenye ualbino na kuweka msukumo wa utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010.

Watanzania wanatakiwa kuachana na imani potofu za kishirikina za kuwaua, kuwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatesa watanzania wenzetu wenye ualbino. Matukio ya ukatili, unyanyasaji, na mauaji kwa watu wenye ualbino yamepungua kwa kiasi nchini. Katika hili Tume inapenda kipekee kutambua juhudi kubwa za Serikali na wadau wote katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino. Wenzetu wenye ualbino wanakabiliwa na changamoto zingine za kielimu, kiafya na kijamii na unyanyapaa ambapo juhudi zaidi kutoka kwa wadau wote zinahitajika. 

Aidha, Tume inaiomba Serikali kuendeleza juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba (sunscreen lotions) na vifaa saidizi vya kielimu kwa watu wenye ualbino ili waweze kushiriki kikamilifu katika kutoa mchango wao katika kujenga Taifa letu. 

Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa nchini.  

 

 

Imetolewa na:

 

Mary Massay

KATIBU MTENDAJI

 

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.