08
Sat, Aug
3 New Articles

THBUB yazitaka AZAKI washirika kujikita kutatua kero za Wananchi

Mkurugenzi wa HUPEMEF, Mchungaji Saimon Chemu (Kulia) akitoa maelezo mafupi kwa Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu (Kushoto) alipotembelea ofisi za Taasisi hiyo zilizopo Wilayani Magu, jijini Mwanza Aprili 21, 2020.

News
Typography

Na Mbaraka Kambona

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu amezitaka taasisi zilizoingia  mkataba wa ushirikiano na Tume kuendeleza jitihada za kusaidia wananchi ili kutatua kero zinazowakabili katika maeneo yao.

Jaji Mwaimu alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano baina ya THBUB na Taasisi ya Huruma, Peace and Mercy Foundation (HUPEMEF) uliofanyika katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Wilayani Magu, Mkoani Mwanza Aprili 21, 2020.

Akiongea katika kikao hicho Jaji Mwaimu alieleza kuwa lengo la THBUB kuingia makubaliano na Taasisi ni kuendelea kusaidia wananchi kupata huduma pale ambapo Tume haiwezi kufika.

“Lengo la ushirikiano ni nyinyi kuisaidia Tume kuwafikia wanachi kule chini ambapo Tume haiwezi kufika, hivyo tuendeleze jitihada zaidi kusaidia wananchi”, alisema Jaji Mwaimu

Aliendelea kuwasisitiza  kuzingatia kazi walizojipangia ili waweze kupata matokea tarajiwa kwa jamii ikiwemo  kuwapunguzia migogoro inayoikabili.  

Aliongeza kuwa Tume inafahamu kazi ambazo taasisi hizo zinazifanya na hivyo itaendelea kushirikiana nazo kupitia mkataba wao wa ushirikiano.

Aidha, Jaji Mwaimu aliishauri taasisi ya HUPEMEF kufanya kazi kwa ukaribu na Ofisi za THBUB zilizopo Kanda ya Ziwa ili waweze kushirikiana katika kutatua migogoro ya wananchi wa eneo la Kanda ya Ziwa.

“Tumieni vizuri Ofisi zetu za Kanda zilizopo hapa Mwanza, msiache kushirikiana nayo, kwa kufanya hivyo kutawasaidia kushughulikia kwa urahisi yale malalamiko ambayo hamna mamlaka nayo na kuyapeleka Tume ambayo ina mamlaka ya kuyashughulikia”, aliongeza Mwaimu

Mkurugenzi wa HUPEMEF, Mchungaji Saimon  Chemu aliishukuru THBUB kwa ziara waliyoifanya katika ofisi hizo na kusema kuwa imewapa nguvu kubwa ya kuendelea kufanya kazi.

“Mwenyekiti tunakushukuru kwa kutuunganisha na Ofisi ya Kanda, tutafanya nayo kazi kwa ukaribu ili tushirikiane nao katika kusaidia wananchi”, alisema Mchungaji Chemu

Jaji Mwaimu alikutana na Uongozi wa Taasisi ya HUPEMEF ikiwa ni sehemu ya ziara yake jijini Mwanza ambayo lengo lake kubwa ni kutembelea ofisi za Tume zilizopo kanda ya Ziwa ili kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa  katika ofisi hizo.

MWISHO.

 

Sign up via our free email subscription service to receive notifications when new information is available.