ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

MWENGE WA UHURU WAZINDUA KLABU ZA HAKI ZA BINADAMU LINDI.

07 May, 2026
MWENGE WA UHURU WAZINDUA KLABU ZA HAKI ZA BINADAMU LINDI.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, amezindua rasmi Klabu za Haki za Binadamu katika shule za sekondari za Hamida Aqussim, Mitwaro na Angaza mkoani Lindi. Uzinduzi huo ni sehemu ya jitihada za kukuza uelewa wa haki za binadamu na utawala bora miongoni mwa vijana.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi iliyofanyika tarehe 03 Mei, 2026 katika Shule ya Sekondari Hamida Aqussim, Ndugu Mwang’onda ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kubuni na kutekeleza wazo la kuanzisha klabu hizo. Aidha, ametoa wito kwa THBUB kuhakikisha inazifikia shule nyingi zaidi ili kuwapa vijana fursa ya kupata elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa manufaa ya Taifa.

“Niwasihi muendelee kuzilea klabu hizi, kwani kupitia vijana hawa tuna matarajio ya kupata viongozi wazalendo, wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora,” amesema Mwang’onda.

Awali, akisoma risala kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Afisa Mfawidhi wa THBUB, Bw. Juma Mleli, amesema kuwa klabu hizo zinatoa jukwaa muhimu kwa wanafunzi kujifunza kwa kina masuala ya haki za binadamu na kushiriki katika shughuli za kijamii zinazochochea mabadiliko chanya.

Ameongeza kuwa, THBUB inaendelea kuanzisha klabu hizo katika shule za msingi, sekondari na vyuo nchini kote kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kuwa mabalozi wa haki za binadamu, maadili mema na uzalendo, na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa lenye usawa na maendeleo endelevu.

Uzinduzi wa klabu hizi unaonesha dhamira ya dhati ya THBUB kuwawezesha vijana kielimu na kimaadili, ili wawe chachu ya mabadiliko chanya katika jamii. Kupitia majukwaa haya, inatarajiwa kuwa kizazi kijacho kitakuwa na uelewa mpana wa haki, wajibu na misingi ya uongozi bora.

slot gacor