ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAFANYA UTAFITI KUHUSU HALI YA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO 

27 Oct, 2026
THBUB YAFANYA UTAFITI KUHUSU HALI YA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO 

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeanza kufanya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Mkoa wa Arusha na Dar es salaam kwa lengo la kubaini ukubwa wa tatizo, vyanzo vyake, aina za ukatili, wahusika, athari zake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na vitendo hivyo.

Akizungumza  Oktoba 19,2026 katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Nyaraka  wa THBUB Bw. Paul Sulle, amesema utafiti huo unalenga kuimarisha hali ya ulinzi wa haki za binadamu nchini.


Bw. Sulle ameeleza kuwa utafiti huo utaiwezesha THBUB kupata taarifa zitakazosaidia kuelewa hali halisi ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo husika, kubaini changamoto zilizopo na kupendekeza hatua stahiki za kuzuia na kukabiliana na vitendo hivyo.


Aidha, Bw. Sulle ameeleza kuwa sambamba na utafiti huo, THBUB itaanzisha klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari ili kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu haki na wajibu wao. Klabu hizo zitatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza namna ya kutambua na kutoa taarifa za vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyowakabili.


Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mkoa wa Arusha, Mwalimu Vincent Kayombo, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Toba Alnason Nguvila, amesema ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha iko tayari kushirikiana na THBUB katika utekelezaji wa utafiti huo.

Bwa. Kayombo amesema matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto mkoani humo.


Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Arusha, Bw. Denice Mgiye, amesema mkoa huo uliripoti matukio 3,400 ya ukatili katika mwaka wa fedha 2025/2026. Ameeleza kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru ina Kituo cha Mkono kwa Mkono kinachotoa huduma bila malipo kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, ikiwemo kusaidia utunzaji wa kumbukumbu na ushahidi.


Aidha, amesema Serikali imeanza mpango wa kujenga kituo kingine katika Wilaya ya Karatu kitakachosaidia kutoa huduma kwa waathirika kutoka wilayani humo na maeneo ya Monduli na Ngorongoro.


Kupitia utafiti huo na uanzishwaji wa klabu za haki za binadamu shuleni, THBUB inalenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu haki za binadamu na kuchangia juhudi za kuzuia ukatili na kujenga jamii inayoheshimu haki na utu wa mtu.

slot gacor