WATUMISHI WA THBUB TAWI LA DAR ES SALAAM WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Tawi la Dar es salaam wametakiwa kuzingatia maadili na kanuni za utumushi wa umma wakati wakitekeleza majukumu yao ili kuweza kukuza heshima ya Tume na Serikali kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa THBUB, Mhe. Nyanda Shuli wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili na uwajibikaji katika utumishi wa umma yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya THBUB, Jijini Dar es salaam Mei 27, 2025
Mhe. Shuli amesema mafunzo hayo ni umuhimu kwa watumishi kwani yatasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kukuza utendaji kazi unaozingatia uwajibikaji na uadilifu.
“Mafunzo haya ni muhimu kwani yatasaidia kutimiza wajibu wetu kama watumishi wa umma na kwamba kanuni za maadili zipo kutuelekeza namna nzuri ya kuenenda sisi kama watumishi wa umma hasa katika jamii zetu.”amesema Mhe. Shuli
Akiwasilisha mada ya Maadili na uwajibikaji katika utumishi wa umma, Bi. Grace Matunda, Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda Maalum ya Dar es Salaam ameeleza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia misingi ya maadili, Sheria na kanuni katika utoaji huduma kwa wananchi.
Aidha, Bi. Grace amesisitiza kuwa watumishi wa umma wanao wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uwazi ili kukuza dhana ya utawala bora nchini.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika kwa lengo la kukuza uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma ili kukuza ubora wa huduma na viwango vya utendaji kazi unaozingatia haki za binadamu na utawala bora.