WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA) ILI KURAHISHA NA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe amezitaka taasisi zote za umma nchini kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza uwajibikaji, ufanisi, kasi na uwazi katika utendaji wa kazi serikalini na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma kwa umma.
Prof. Shemdoe amesema hayo wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka katika Kilele cha Maadhimissho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma Juni 23,2026.
Prof. Shemdoe amesema kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yamekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza uwazi na kupunguza gharama za utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Utumiaji wa mifumo itasaidia kuunganisha mawasiliano baina ya taasisi na taasisi na kuongeza uwazi, uwajibikaji pamoja na utawala bora” amesema Prof. Shemdoe.
Katika hafla hiyo Pro. Shemdoe alizindua mifumo ya GSD na NGAO inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za Serikali na kuimarisha usalama wa mifumo ya kidijitali serikalini.
"Mfumo huo utawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za serikali kupitia dirisha moja kwa urahisi" amesema Prof. Shemdoe.
Maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma yalianza Juni 16 hadi 23, 2026 ambapo lengo ni kutambua mchango wa watumishi wa katika kutoa huduma kwa wananchi.

