ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

WAZIRI MKUU AIPONGEZA WIZARA YA KATIBA

23 Jun, 2025
WAZIRI MKUU AIPONGEZA WIZARA YA KATIBA

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezipongeza Wizara za Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutekeleza kikamilifu na kwa ufanisi maono ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watanzania wanapata haki zao za Kikatiba.

Mhe. Majaliwa ametoa pongezi hizo leo Juni 16, 2025 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika katika viwanja vya Maturubai Mbagala Jijini Dar es salaam.

“Niwapongeze Mawaziri wa Katiba na Sheria kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kule Zanzibar kwa kuendelea kusimamia kwa ufanisi maono ya Kiongozi wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwafanya watanzania waanze kutambua haki zao lakini pia kujua sheria zinazoweza kuwalinda na kulinda maslahi yao “ amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika uzinduzi huo Waziri Mkuu Majaliwa alisema Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya kisheria bila kikwazo chochote cha kiuchumi hivyo kuchochea maendeleo endelevu.

Aliongeza kuwa kampeni hii itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

Aidha, Mhe. Majaliwa amewataka wananchi wote wenye changamoto mbalimbali za Kisheria kujitokeza kwa wingi kwenye siku kumi za utekelezaji wa kampeni hiyo kwa mkoa wa Dar es salaam.

Katika hatua nyingine Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeshiriki katika uzinduzi huo ambapo wananchi wamefika katika banda la THBUB na kupatiwa elimu ya haki za  binadamu na utawala bora, kupatiwa msaada wa kisheria pamoja na kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Uzinduzi huo wa Msaada wa kisheria wa Mama Samia una kauli mbiu isemayo “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo “.