SERIKALI YAIMARISHA UPATIKANAJI WA HAKI KWA WAFUNGWA NA MAHABUSU
Serikali imechukua hatua ya kuimarisha ulinzi wa haki za wafungwa na mahabusu nchini kwa kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria magerezani, kuongeza uelewa wa haki na kuimarisha usimamizi wa mashauri.
Hati hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndugu Ali Gugu Jijini Dar es Salaam Leo Oktoba 27, 2026 na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi na Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu, Bw. Patience Ntwina.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mhe. Ulega, amesema ushirikiano huo utaimarisha uratibu wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu.
Aidha, Mhe.Ulega ameeleza kuwa upatikanaji wa haki haupaswi kutegemea uwezo wa kiuchumi wa mtu, akisisitiza kuwa wafungwa na mahabusu wanapaswa kupata msaada wa kisheria bila kujali hali zao za kiuchumi. Kauli hiyo inasisitiza umuhimu wa kulinda utu wa binadamu na kuimarisha misingi ya usawa mbele ya sheria.
Kwa upande wake, Mhe. Katambi, amesema makubaliano hayo yatawasaidia wafungwa na mahabusu kuelewa haki zao, taratibu za kisheria na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika mashauri yao.
Akieleza matokeo ya huduma za msaada wa kisheria zilizotolewa nchini, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu, amesema kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, jumla ya wafungwa na mahabusu 19,511 katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Ruvuma, Singida na Njombe wamenufaika na huduma hizo.
Aidha, Katungu amesema watumishi zaidi ya 290, wakiwemo maafisa sheria, maafisa urekebu na wasaidizi wa kisheria, wamepatiwa mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kutoa huduma hizo kwa ufanisi. Mafunzo kwa watoa huduma yatachangia kuchangia kuboresha ubora wa ushauri wa kisheria na kurahisisha utambuzi wa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na utiaji saini wa hati hiyo, Mhe. Ulega na Mhe. Katambi wamezindua Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Madawati ya Msaada wa Kisheria Magerezani, unaolenga kuimarisha uratibu na usimamizi wa huduma hizo.kuweka utaratibu wa kuwafikia wafungwa na mahabusu wanaohitaji msaada wa kisheria, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za haki jinai.

