ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

DK. MWINYI AWAHIMIZA WANAWAKE KUTUMIA HAKI YAO YA KUGOMBANIA UONGOZI

09 Mar, 2025
DK. MWINYI AWAHIMIZA WANAWAKE KUTUMIA HAKI YAO YA KUGOMBANIA UONGOZI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za Uongozi muda utakapowadia ili kutimiza haki yao ya msingi.

Dk. Mwinyi amesema hayo alipozungumza kwenye Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliofanyika viwanja vya Maonesho Dimani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 06 Machi, 2025.

Aidha, amepongeza kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani na kueleza kuwa inasisitiza haja ya kuwekeza kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali vya wajasiriamali wanawake na kupambana dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Pia, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kuongeza idadi ya wanawake kwenye uongozi wake, kwa ngazi zote wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, na Wakurugenzi. 

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yenye kauli mbiu  "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki Usawa na Uwezeshaji" mbali na Rais Dk. Mwinyi, pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, viongizi wengine wa Serikali na wawakilishi wa taasisi za kimataifa.