WANAWAKE WA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Watumishi wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wameungana na wanawake wengine kutoka taasisi za Serikali na binafsi kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026 katika maeneo mbalimbali nchini.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika matawi tofauti ikiwemo Mtwara katika viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam katika viwanja vya Barafu Ubungo, Mwanza katika viwanja vya Nane Nane Kisesa, huku kwa upande wa Dodoma yakifanyika katika viwanja vya Shule ya Mbande wilayani Kongwa, ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho ya Dodoma alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo: “Haki kwa wanawake na wasichana ni msingi wa maendeleo jumuishi kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.” Kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na fursa sawa katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, uchumi, uongozi na ushiriki katika maamuzi ya maendeleo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo jijini Dodoma, Mheshimiwa Senyamule alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda na kutetea haki za wanawake na wasichana, akieleza kuwa jamii ina wajibu wa kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubaguzi na unyanyasaji vinatokomezwa ili kuweka mazingira salama na yenye usawa kwa wote.
Kwa upande wa THBUB, ushiriki wa watumishi wanawake wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika maadhimisho hayo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuendelea kuhamasisha ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu, hususan haki za wanawake na wasichana. Kupitia majukumu yake ya kikatiba, Tume inaendelea kutoa elimu kwa umma, kupokea na kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kushauri Serikali na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kuimarisha utawala bora na usawa katika jamii.
Kupitia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, jamii imekumbushwa kuwa kulinda na kuheshimu haki za wanawake na wasichana si wajibu wa wanawake pekee bali ni jukumu la jamii nzima, hatua ambayo ni muhimu katika kujenga taifa lenye usawa, haki na maendeleo jumuishi

