UTUMISHI WA UMMA UNAHITAJI UWAJIBIKAJI NA BIDII YA KAZI
wa Umma Unahitaji Uaminifu, Uwajibikaji na Bidii ya Kazi”Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali Watu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, (THBUB) Bw. Johnston Mwakalitolo, amewataka watumishi wa Tume kuzingatia maadili ya kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Bw. Mwakalitolo ametoa wito huo leo Machi 5, 2025 wakati wa ziara yake katika Tawi la Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa utumishi wa umma unahitaji watumishi wenye uaminifu, uwajibikaji na bidii katika kutekeleza majukumu yao.
“Mtumishi wa umma anatakiwa kufanya kazi kwa haki, kuheshimu wananchi na kutumia rasilimali za umma kwa uangalifu ili kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.” amesema Bw. Mwakalitolo
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Tawi la Dar es Salaam, Bi. Shoma Philip, amesema kuwa watumishi katika tawi hilo wanaendelea kufuata kanuni za maadili ya kazi kwa kuwahudumia wananchi kwa heshima na kwa haki.
Aliongeza kuwa tawi hilo linaendelea kuwahamasisha watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na kutumia rasilimali za umma kwa uangalifu.
Aidha, Watumishi wa THBUB Tawi la Dar es Salaam walimshukuru Bw. Mwakalitoto kwa ziara yake pamoja na maelekezo aliyoyatoa, wakieleza kuwa yamewapa hamasa na mwelekeo zaidi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Waliahidi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa uaminifu, uwajibikaji na bidii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haki na kwa wakati.

