ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

UTANGULIZI


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya Serikali, iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania.

THBUB ilianzishwa chini ya Ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 3 ya mwaka 2000.A

Tume ilianza kazi Julai 1, 2001 baada ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura ya 391 na Tangazo la Serikali Na. 311 la Juni 8, 2001. Tume ilizinduliwa rasmi Machi 15, 2002 baada ya kuteuliwa na kuapishwa kwa Makamishna wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Tume ilianza kazi rasmi Aprili 30, 2007 baada ya Sheria ya THBUB Sura ya 391 kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi kwa kutungiwa Sheria Na. 12 (Extension Act) ya Mwaka 2003.

Eneo la Utoaji Huduma

THBUB inatoa huduma zake katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mitano (5) ya Zanzibar kupitia ofisi yake kuu iliyoko Dodoma na Unguja; vile vile kupitia ofisi zake za kanda zilizoko Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Pemba.

THBUB inaendelea kufanya jitihada ili kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa kufungua ofisi nyingi zaidi za matawi nchini.

Ubia

Tunaamini katika usemi usemao: “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.” Moja ya mambo makubwa THBUB inayojishughulisha nayo ni kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali. Tunaamini kuwa masuala ya haki za binadamu yaliyopo nchini Tanzania yanaweza kushughulikiwa vyema iwapo tu utakuwepo ushirikiano mzuri miongoni mwa wadau.

Hadi sasa THBUB imesaini mikataba ya makubaliano ya ushirikiano na Asasi 31 Zisizo za Kiserikali katika utoaji wa elimu ya haki za binadamu na utawala bora nchini. Uhusiano bora hauishii katika kushirikishana mawazo na uzoefu tu miongoni mwa wadau, bali pia kuwa tayari kushirikishana rasilimali muhimu zinazohitajika katika utekelezaji wa malengo ya pamoja.

Tume iko tayari kushirikishana rasilimali hizo na wadau wengine wote wanaojitahidi kufanya dunia iwe mahali bora pa kuishi. Iwapo ungependa kuwa sehemu ya mahusiano haya yanayokuwa siku hadi siku, unaweza kushirikiana nasi kwa kuwasiliana nasi kwa anwani na namba za simu zilizooneshwa hapa chini.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Kitalu Na. 339 Mtaa wa Nyerere/Kilimani

S.L.P 1049, DODOMA

Simu: +255 734 047 775; 734 119 978

Barua Pepe: info@chragg.go.tz

Tovuti: www.chragg.go.tz