THBUB ya waasa Watendaji Kata na Vijiji kuzingatia utawala bora

Watendaji wa Kata na Vijiji wahimizwa kutenda haki na kuzingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo ameyabainisha Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Watendaji hao ,yaliyofanyika
Januari 16,2024 katika Ukumbi wa Isawima, Wilaya ya Kaliua ,Mkoani Tabora.
Mhe. Mohamed alisema kuwa Watendaji wa Kata na Kijiji ni daraja la kuunganisha Serikali na Wananchi ili kuinua maendeleao kwa pamoja hivyo Watendaji hao wanapaswa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa kuzingatia sheria zilizoekwa ili kusimamia na misingi ya utawala bora utakaosaidia kuleta maendeleo katika Jamii.
Pia Mhe.Mohamed alieleza kuwa kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kuwa Watendaji kutokuwashirikisha wananchi ikiwemo kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya Kata na Kijiji ili kuimarisha msingi wa uwazi na kuondoa sintofahamu kwa wananchi kuhusu matumizi ya fedha za maendeleo.
“Kumekuwa na changamoto nyingi katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na wananchi kutopewa taarifa ya mapato na matumizi ya Kijiji ,kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki na kukiuka misingi ya utawala bora” alisema Mhe. Mohamed
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua Bw. Raymond Mweli amewataka Watendaji hao kutenda haki kwa Jamii pamoja na kuwaelimisha juu ya haki na wajibu wao.
“Mafunzo mtakayopata mtumie kama njia ya kuongeza ufanisi na uadilifu kwenu na Jamii kwa ujumla”alisema Bw. Mweli
Katika Ziara hiyo THBUB imetoa mafunzo ya haki za binadamu na misingi ya utawala pamoja na kuzindua Klabu ya Haki za Binadamu katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii na Shule ya Sekondari Kaliua
Aidha,THBUB imefanya mkutano wa hadhara na kupokea kero mbalimbali za wananchi wa Kata ya Ufukutwa