ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU NI SILAHA YA KUJENGA TAIFA LENYE UTAWALA BORA

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) ametoa rai kwa Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na misingi ya utawala bora inaimarishwa nchini ili kujenga Taifa lenye utawala bora.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Waislamu Ahmadiyya nchini Tanzania uliofanyika leo Septemba 27, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mwaimu alisema Tume imeendelea kuwa chombo cha kuaminika kwa wananchi kwa kupokea na kushughulikia malalamiko, kutoa elimu ya uraia na kufuatilia utekelezaji wa sheria na sera zinazohusu haki na wajibu wa binadamu.
“Tume imeendelea kuwa chombo cha kuaminika kwa wananchi kwa kupokea na kushughulikia malalamiko, kutoa elimu ya uraia na kufuatilia utekelezaji wa sheria na sera zinazogusa haki na wajibu wa binadamu,” alisema Mwaimu.
Aliendelea kwa kuishukuru Jumuiya hiyo kwa kueneza amani, upendo, ushirikiano, kuhimiza utii wa sheria kwa dini zote, kuhimiza maadili mema kupitia mafundisho ya Dini ya Kiislam pamoja na kutoa huduma za kijamii kama vile maji na elimu.m, kwani hivyo vyote vinahusiana na ulinzi na uzingatiwaji wa haki za binadamu zinazotamkwa katika Katiba na Sheria zetu pamoja na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia.
Aidha, Mhe. Mwaimu amesisitiza kuwa haki ya kuabudu ni miongoni mwa haki za msingi zinazolindwa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 19 ya Katiba hiyo inatoa uhuru kwa kila mtu kuamini, kuabudu na kushiriki katika dini au imani anayoichagua bila kulazimishwa au kubaguliwa.
Kwa upande wake, Sheikh Khawaja Muzafar Ahmad, ambaye ni Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislam Ahmadiyya, alimshukuru mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo na kueleza kuwa dhamira kuu ya mkutano ilikuwa ni kutoa elimu juu ya haki za binadamu kwa misingi ya Kiislamu.
“Lengo la mkutano huu ni kujifunza haki za binadamu kwa misingi ya Kiislamu, namna ya kuzidai, wajibu wa Muislamu katika kupata na kulinda haki yake, pamoja na namna ya kuishi kwa kuzingatia haki za wengine na viumbe wengine,” alisema Sheikh Ahmad.
Mhe. Mwaimu alimalizia hotuba yake kwa kubainisha kuwa Tume itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na haki zake za msingi na taifa linaendelea kujengwa juu ya misingi ya haki, utu na demokrasia.