THBUB YAHIMIZA WANAWAKE WAVUVI KUZIJUA ,KUZILINDA NA KUDAI HAKI ZAO
Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Patience Ntwina, amewahimiza wanawake wavuvi nchini kuelewa na kudai haki zao za msingi ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya uvuvi.
Bw. Ntwina ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), yaliyoandaliwa na THBUB kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark (DIHR), yaliyofanyika Februari 5 hadi 6, 2026, Mjini Morogoro.
Akielezea lengo la mafunzo hayo, Bw. Patience Ntwina, amesema kuwa lengo kuu la mafunzoUB YAHU ni kuwawezesha wanawake wavuvi kuelewa haki zao za msingi, kuzidai pale zinapokiukwa, na kuwa mabalozi wa utetezi wa haki za binadamu katika jamii zao.
“THBUB ina wajibu wa kuhakikisha haki za binadamu zinakuzwa, zinalindwa na kuhifadhiwa kwa usawa katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni, hususan kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi kama wanawake wavuvi wadogo,” amesema Bw. Ntwina.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Margrethe Dominic, Akizungumza katika mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema kuwa sekta ya uvuvi nchini Tanzania inategemea zaidi wavuvi wadogo wanaofikia asilimia 90, huku wanawake wakichangia kwa kiwango kikubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Aidha, Mwenyekiti wa TAWFA Taifa, Bi. Beatrice Mmbaga, amesema kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo wanaishukuru THBUB kwa kuandaa mafunzo hayo na kwamba kupitia THBUB washiriki wamepata elimu kuhusu misingi ya haki za binadamu, mbinu za utetezi, usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji, pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko katika mamlaka husika ikiwemo THBUB.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha viongozi wa TAWFA kutoka maeneo mbalimbali ya uvuvi ikiwemo bahari, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika, pamoja na vyanzo vidogo vya maji. Pia yalihusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), pamoja na watumishi wa THBUB.

