WATUMISHI THBUB WATAKIWA KUTAMBUA HAKI NA WAJIBU WAO.
Watumishi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wametakiwa kutambua haki na wajibu wao, kuzingatia maadili ili kuleta utendaji wenye tija, staha na heshima mahala pa kazi.
Hayo, amesema Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patience Ntwina wakati akifungua Mkutano wa ishirini na nne wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika Februari 11, 2026 ukumbi wa NALA Hoteli, Jijini Dodoma.
Bw. Ntwina amesema kuwa Baraza la Wafanyakazi ni Chombo muhimu kinacho wawezesha watumishi kupitia wawakilishi wao kujadili masuala yanayohusu maslahi yao na mahusiano ya kazi kwa Pamoja.
“Mabaraza haya yameundwa kisheria kama vyombo vya ushauri katika Taasisi kwa lengo la kuongeza tija, kuimarisha mshikamano kati ya watumishi na mwajiri sambamba na kutekeleza wajibu ili kufikia malengo.
Pia, Bw. Ntwina ameeleza kuwa mkutano huo unalenga kujadili utekezaji wa majukumu ya THBUB kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya mafungu madogo kwa mwaka 2026/2027.
“Ni mategemeo yangu kuwa wajumbe mtajadili kwa makini na kutoa maoni yenye kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yetu na kufikia malengo ya taasisi” amesema Bw. Ntwina
Aidha, Bw.Ntwina ametoa wito kwa wajumbe hao kujadili kwa kina malengo na mipango ya THBUB, ikiwemo maslahi ya watumishi, njia za kuboresha utendaji kazi ili kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi waonahitaji huduma kutoka THBUB.
“Niwaombe majadiliano haya yaongozwe na hekima, busara, uwazi na maelewano yatakayotatua changamoto zetu” amesema Bw. Ntwina

