HAKI ZA BINADAMU NI MAISHA

Katika kuhakikisha maisha yenye utu yanazingatiwa, kila mtu ana haki ya kuishi kwa heshima kwa kupata huduma muhimu kama afya, elimu, chakula, makazi bora, ajira ya staha na usalama.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mohamed Khamis Hamad wakati akifungua mkutano wa Wadau kuhusu uhakiki wa haki za binadamu katika shughuli za biashara ulifanyika katika ukumbi wa hotel ya PH Mkoani Morogoro, Agosti 19, 2025.
Mhe. Mohamed amewakumbusha
Akizungumza na wadau walio hudhuria mkutano huo, Mhe. Mohamed amewasihi wakumbuke wajibu wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu katika maeneo ya biashara.
“Biashara kama chanzo cha ajira na maendeleo ya kiuchumi zinategemea sana uzingatiaji wa haki za binadamu” Alieleza.
Naye Katibu Mtendaji wa THBUB, Bw. Patience Ntwina alieleza lengo la mkutano huo kuwa ni kuwajengea uwezo wadau, kutambua, kuhakiki, kuzuia na kushughulikia athari za haki za binadamu zinazoweza kusababishwa na shughuli za kibiashara.
Wadau kutoka sekta binafsi walisisitiza kwamba ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango kazi wa Kitaifa wa haki za binadamu na Biashara.
Wadau hao wamesema kuwa mazingira bora ya biashara hujengwa pale ambapo haki zinalindwa ipasavyo.
Mkutano huo umeandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ya Denmark ambayo imewakilishwa na Bw. Bernard Ochieng kutoka Kenya, umehusisha wadau kutoka Makampuni ya sekta ya uzalishaji, kilimo, usafirishaji na Taasisi simamizi za biashara.