ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU THBUB YAWAKUMBUSHA WANAHABARI KUTOKUWA SEHEMU YA UVUNJIFU WA AMANI

25 Sep, 2025
KUELEKEA UCHAGUZI MKUU THBUB YAWAKUMBUSHA WANAHABARI KUTOKUWA SEHEMU YA UVUNJIFU WA AMANI

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa wito kwa waandishi wa habari kujiepusha na lugha za uchochezi zenye kuleta taharuki kwenye jamii hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa 2025.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa tume hiyo, Khatibu Mwinyichande alipofungua mafunzo ya siku moja yaliyohusu haki za binaadamu na wajibu wa waandishi wa habari wakati wa uchaguzi mkuu 2025.

Mafunzo hayo yalifanyika ukumbi wa Baraza la Manispaa, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, tarehe 20 Septemba, 2025.

Katika nasaha zake kwa waandishi hao, Kamishna Mwinyichande aliwasihi kuandika habari zitakazolenga kudumisha amani katika nchi na kuondosha migogoro itakayotokana na taarifa zitakazotolewa na vyombo vyao.

“Katika kipindi cha uchaguzi Waandishi wa habari mnatakiwa kutumia kalamu zenu kuelimisha na sio kuharibu hasa kipindi tulichonacho kuelekea uchaguzi mkuu, 2025,”  alisema Kamishna Mwinyichande.

Aidha, alieleza mwanahabari mzuri ni yule mwenye kutangaza mema yanayofanywa ndani ya nchi yake na kujiletea mafanikio.

Pia Kamishna Mwinyichande aliwatanabahisha waandishi hao kutoegemea upande wa chama kimoja na kutoa udhaifu wa vyama vyengine.

Pia, alieleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa waandishi hao majukumu ya kuhabarisha na kuelismisha jamii kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo haki za binaadamu na misingi ya utawala bora wakati wa uchaguzi mkuu wa 2025.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa THBUB, Juma Msafiri Karibona aliwaeleza waandishi hao kuwa wana nafasi kubwa ya kuhubiri amani na mshikamano kuelekea na baada ya uchaguzi mkuu.

Aliwaeleza waandishi hao kwamba taarifa watakazozitoa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, zitahitaji ufanisi na usahihi ili kuondosha mifarakano katika jamii.

Akiwasilisha mada kwa waandishi hao iliyosema “Haki na wajibu wa waandishi wahabari wakati wa uchaguzi”, Afisa Uchunguzi kutoka THBUB ofisi ya Dar es Salaam, Tunu Myenda, aliwaeleza waandishi hao kwamba wana nafasi kubwa kwa jamii ya kuelimisha kupia fani yao.

Aliwaeleza kupitia taaluma yao wana uwezo wa kulinda haki ama kuwa sehemu ya uvunjifu wa haki hizo, hivyo aliwaelezea wajibu wao wa kulinda haki hizo ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza endapo waandishi wa habari watatoa taarifa za kupotosha, Tunu alisema ni pamoja na kupoteza imani kwa vyombo vya habari, wananchi kufanya maamuzi mabaya kisiasa na kiuchumi kunatokana na kuamini taarifa za uongo pamoja na taarifa kuchafua jina la mtu, Shirika au Serikali.

THBUB inatoa mafunzo ya aina hiyo kwa waandishi wa habari wa mikoan 14 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar  kwa Unguja na Pemba, ili kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu, wajibu wa vyombo vya habari na nafasi yao katika kulinda haki za binadamu.