ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

Mamlaka zatakiwa kutekeleza mapendekezo ya THBUB kwa wakati

14 Mar, 2024
Mamlaka zatakiwa kutekeleza mapendekezo ya THBUB kwa wakati

Wito umetolewa kwa mamlaka mbalimbali zinazopokea mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kutekeleza mapendekezo hayo kwa wakati na kutoa mrejesho.

Wito huo umetolewa leo Machi 13, 2024 na Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu) alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja baina ya Tume na wawakilishi wa mamlaka za Serikali uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.

Wawakilishi hao walikutana maalum kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya Tume kufuatia chunguzi kadhaa za malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mheshimiwa Mwaimu aliwaeleza wajumbe wa mkutano kuwa taasisi yake ilifikia uamuzi wa kukutana na mamlaka hizo kutokana na mwitikio mdogo katika utekelezaji wa mapendekezo yake.

“THBUB imeona kuna haja ya kukutana pamoja na kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwa taasisi zenu," Mheshimiwa Mwaimualisema, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na Mheshimiwa Mwenyekiti Tume inao wajibu wa kufuatilia mapendekezo yake katika mamlaka husika kwa kuwasiliana na mamlaka hizo kwa njia mbalimbali, ikiwemo barua,simu,kukutana ana kwa ana na watendaji wa mamlaka hizo kwa kufika katika ofisi zao na katika mikutano kama hiyo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Wawakilishi kutoka Halmashauri ya Mji wa Muheza,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,TAKUKURU,na Jeshi la Polisi.

Wajumbe wengine walitokaOfisi ya Taifa ya Mashtaka,Wizara ya Katiba na Sheria,Wizara Mambo ya Ndani ya Nchi,Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),na Ofisi ya Waziri Mkuu.