SHUGHULI ZA KIBIASHARA ZIENDE SAMBAMBA NA HAKI ZA BINADAMU

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Khamis Hamad ametoa wito kwa Serikali, taasisi, na wafanyabiashara nchini kuhakikisha kuwa shughuli zote za kibiashara zinafanyika kwa kuzingatia ulinzi na kuheshimu ya haki za binadamu.
Alizungumza hayo alipo tembelea Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam Julai 6, 2025.Mhe. Hamad alisema kuwa haki za binadamu zina mawanda mapana yanayojumuisha pia sekta ya biashara.
"Ni muhimu shughuli za kukuza uchumi zifanyike kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora. Kinyume na hapo, huleta athari kwa jamii, ikiwa ni pamoja na migomo pale wafanyakazi wanapokosa mishahara, hali ambayo hushusha ustawi wa biashara na uchumi wa nchi kwa ujumla," alisisitiza Mhe. Hamad.
Ameongeza kuwa Tume imekuwa ikishughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa haki za binadamu kwenye shughuli za biashara na tayari Tume imewasilisha kwa Serikali rasimu ya Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara ikiwa ni hatua ya kuimarisha ulinzi wa haki hizo katika sekta hiyo.
"Katika rasimu hiyo tumeainisha vipaumbele kumi na moja vikiwemo haki katika ajira, usimamizi wa ardhi na maliasili, pamoja na ulinzi wa mazingira kwani Changamoto kubwa ya uvunjwaji wa haki za binadamu hutokana na uelewa mdogo wa wadau kuhusu masuala haya muhimu," alieleza Kamishna Hamad.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeendelea kushiriki maonesho hayo yenye kaulimbiu "Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania", kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kufanya biashara kwa kuzingatia haki za binadamu, kusikiliza na kutatua malalamiko ya uvunjaji wa haki hizo, na kuimarisha misingi ya utawala bora nchini