THBUB LETENI MALALAMIKO YENU YAUVUNJIFU WA HAKI WANANCHI

Kisiwani Pemba wameshauriwa kuyafikisha malalamiko yao ya kisheria, yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, (THBUB), ili kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
Hayo yameelezwa na Mwanasheria kutoka THBUB Bw. Mohammed Masoud hivi karibuni wakati akielezea majukumu ya tume, kwenye mikutano ya wazi iliyoandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Sheria, Zanzibar katika kijiji cha Mlalashi, Shehia ya Mjanaza, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Bw. Masoud amesema moja ya jukumu la THBUB ni kupokea na kusikiliza malalamiko mbalimbali ya uvunjifu wa haki wa binadamu na misingi ya utawala bora, bila ya malipo yoyote.
Aidha, Bw. Masoud ameeleza moja ya kazi ya THBUB ni kujenga uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa haki za binadamu kwa kuzingatia misingi ya utawala bora kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“ Kwa mfano umevunjiwa nyumba yako, kwa kupisha mradi wa kijamii kama barabara au ujenzi wa skuli na hakuna dalili ya kulipwa fidia, njoo tutashirikiana” alisema.
Akiwaelekeza namna ya kuwasilisha malalako Bw. Masoud amesema kwa sasa ofisi za THBUB kisiwani Pemba zipo Chake chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika hatua nyingine, Masoud aliwataka wananchi hao, wasiwe chanzo cha kuvunjiana haki miongoni mwao, ikiwemo kuzifanyia suluhu kesi za jinai.
‘’Imekuwa kawaida, kunapotokea kesi za ubakaji kwenye jamii, familia hukaa pamoja na kutafuta suluhu, ikiwemo kuwafungisha ndoa waliodhalilishana, jambo ambalo ni kosa jingine, kisheria’’alifafanua.
Mwanasheria huyo pia aliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la UNDP kufanikisha mikutano hiyo kwa baadhi ya shehia kisiwani Pemba, zikiwemo Shehia za Mbuzini na Mchanga Mrima za Wilaya ya Chakechake, na Shehia za Mgagadu na Minazini kwa Mkoa wa Kusini Pemba.