ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YALITAKA JESHI LA POLISI KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU WAKATI WA UCHAGUZI MKUU

22 Sep, 2025
THBUB YALITAKA JESHI LA POLISI KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU WAKATI WA UCHAGUZI MKUU

Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Philipo Raphael Sungu, amesisitiza wajibu mkubwa wa Jeshi la Polisi kuhakikisha amani, utulivu na ulinzi wa haki za binadamu katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Akizungumza katika mafunzo kwa Maafisa wa Polisi mkoani Kigoma, Septemba 20,2025, Bw. Sungu alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa kutoshiriki migogoro, kutoegemea upande wowote, na kulinda misingi ya utawala bora.

“Jeshi la Polisi lina wajibu wa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima, kuhakikisha mazingira wezeshi kwa uchaguzi huru na wa haki, na kuimarisha utii wa sheria bila ubaguzi,” alisema Bw. Sungu.

Kwa upande wake, Afisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB, Bw. Raphael Mavunde, alionya kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi unaweza kuathiri heshima ya taifa kimataifa, kudhoofisha mahusiano na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, na hata kusababisha machafuko yenye madhara makubwa kwa jamii.

Naye, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kasulu, SSP Haji, akimwakilisha Mkuu wa Kituo cha Polisi Uvinza, SP. Kubebeka K. M, aliishukuru THBUB kwa mafunzo hayo muhimu na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litayazingatia kwa mujibu wa sheria na taratibu. Alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wanatimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi kwa amani na utulivu.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili yalijumuisha Maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka Kigoma Mjini, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Kasulu.