emblem

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu

Habari

THBUB YATOA MSAADA WA MAGODORO GEREZA LA ISANGA NA ZAHANATI YA IHUMWA JIJINI DODMA.


Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora walioko Ofisi za Makao Makuu wametoa msaada wa magodoro kumi (10) kwa Gereza Kuu la Isanga, magodoro matano (5) pamoja na vifaa vya kupima uzito watoto katika Zahanati ya Ihumwa Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa huo, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Mhe. Dkt. Fatma R. Khalfani alisema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaadhimisha Siku ya Wanawake kwa namna tofauti kwa kuifikia jamii na kutoa elimu, kuwatembelea na kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji.

“...Wiki iliyopita tulienda Shule ya Sekondari Dodoma na leo tumekabidhi magodoro, kifaa cha kupimia uzito watoto pamoja na chombo cha kuwekea taka” Alisema Mhe. Dkt. Fatma.

Mhe. Dkt. Fatma alisema , Tume itaendelea kushirikiana na jamii katika kutoa elimu juu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kujenga kizazi chenye haki na usawa. Aidha Dkt. Fatma alitoa wito kwa jamii kuendeleza utamaduni wa kutoa kwa kidogo mtu alichobarikiwa kwa ajili yawatu wenye uhitaji.

“Watu wanafikiri mpaka uwe na kitu kikubwa, haba na haba hujaza kibaba. Wote tunajenga nyumba moja, sadaka ni kitu kikubwa. Yule anaetoa anafaidika kuliko anaepokea” Alisema Dkt. Fatma.

Kwa upande mwingine Dkt. Fatma aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar kwa kuendeleza na kusimamia haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

“...Sisi kama Tume jukumu letu kubwa ni kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini” Alisema Dkt. Fatma.

Kwa upande wake Bi. Thabita Joseph, Muuguzi katika Zahati ya Ihumwa alishukuru uongozi wa THBUB pamoja na watumishi wake kwa kuwapelekea magodoro na vifaa vya kupimia uzito watoto.

“...Awali tulikua na magodoro matatu (3) ambayo yalikuwa hayatoshelezi. Kwa kupokeamagodoro haya mapya, yatatusaidia” Alisema Bi. Thabita.