THBUB YAWAKUTANISHA WAANDISHI WA HABARI WA MKOA WA MARA, YAWATAKA KUZINGATIA WELEDI KATIKA KUHABARISHA UMMA.
Waandishi wa Habari Mkoani Mara wametakiwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi yao katika kuhabarisha Umma hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili kulinda haki za binadamu na amani ya nchi.
Wito huo umetolewa leo Septemba 19, 2025 na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Dkt. Thomas Masanja wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara katika mafunzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jeshi la polisi Mkoa wa Mara yaliyolenga kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari kuhusu haki za binadamu na wajibu wao katika kuhabarisha Umma.
Akizungumza katika mafunzo hayo Dkt. Masanja amesema waandishi wa habari wana jukumu la msingi la kutoa taarifa sahihi na zisizo na upendeleo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na haki na kusisitiza kuwa endapo watatumia vibaya kalamu zao wanaweza kuwa chanzo cha ukosefu wa amani.
"Waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya Tume na jamii, ni wajibu wenu sasa kuhakikisha taarifa mnazotoa zinazingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora, ili kuepuka maneno ya uchochezi na kuleta utulivu nchini, ndio maana tumewaita hapa ili tuelekezane namna bora ya kulinda haki na amani kupitia kalamu zenu" amesema Dkt. Masanja.
Dkt. Masanja ameongeza kuwa, mafunzo haya yatafungua ukurasa mpya kwa waandishi katika kuripoti matukio ya uchaguzi Mkuu kwa weledi, ikiwemo kuepuka lugha zisizorafiki na namna ya kutambua matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na namna ya kuripoti matukio hayo kwa njia salama na yenye tija huku akiwataka waandishi wa habari kuwa walimu kwa jamii katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

