THBUB YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MATUMIZI MABAYA YA HABARI WAKATI WA UCHAGUZI MKUU

Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Philipo Raphael Sungu, amewataka waandishi wa habari kuwa makini na tahadhari kubwa dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika mafunzo kwa waandishi wa habari wa Kigoma Mjini yaliyohusu wajibu wa Waandishi wa Habari katika Uchaguzi Mkuu, Bw. Sungu alisema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini kwa kutumia kalamu zao ipasavyo na kuepuka kuchochea vurugu, chuki na ubaguzi.
Kwa upande wake, Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka THBUB, Bw. Said Zuberi, aliwakumbusha waandishi wa habari kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na kimaadili muda wote wa uchaguzi. Alisisitiza kuwa kuna sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia uchaguzi ambazo waandishi wanapaswa kuzielewa na kuzifuata ili kuepusha migongano na vyombo vya dola.
Aidha, Bw. Zuberi alibainisha mambo muhimu ambayo waandishi wanapaswa kuzingatia katika kuripoti habari za uchaguzi, ikiwemo Kutoa uwiano sawa wa taarifa kwa vyama na wagombea, kuripoti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, kuheshimu sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi, kuhubiri amani na utulivu pamoja na kuepuka lugha ya matusi, kejeli, upotoshaji na habari zenye kuchochea vurugu au chuki.
Pia alikumbusha kuwa ni muhimu waandishi wa habari kuhakikisha wamesajiliwa na kuthibitishwa na Bodi ya Ithibati kabla ya kuripoti habari za uchaguzi ili kuhakikisha uwajibikaji na weledi.
Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa na uwajibikaji wa waandishi wa habari wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kitaifa katika kipindi cha uchaguzi mkuu