THBUB YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUEPUKA UCHOCHEZI KIPINDI CHA UCHAGUZI

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanazingatia maadili ya taaluma yao kwa kuepuka kuchapisha au kusambaza taarifa zenye mwelekeo wa uchochezi na upotoshaji, hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu haki na wajibu wa waandishi wa habari katika uchaguzi, Katibu Mtendaji wa THBUB Bw. Patience Ntwina alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa kwa kutoa taarifa sahihi, zenye uwiano na zinazozingatia maadili ya kitaaluma.
“Ni wajibu wa kila mwandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya nchi kwa kuepuka lugha za uchochezi na taarifa za upotoshaji ambazo zinaweza kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi,” alisema Bw. Ntwina
Aidha, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuhakikisha wanazingatia misingi ya weledi, uadilifu na haki za binadamu katika kazi zao, akibainisha kuwa umma unategemea habari sahihi ili kufanya maamuzi bora katika kipindi cha uchaguzi.
THBUB imeendelea kusisitiza kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kujenga demokrasia jumuishi na yenye amani, hivyo vina wajibu wa kuunga mkono jitihada za taifa kulinda mshikamano wa kitaifa na kuepusha migogoro inayoweza kusababishwa na taarifa zisizo sahihi.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuongeza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu haki na wajibu wakati wa uchaguzi ili kuwawezesha kuripoti kikamilifu maudhui ya uchaguzi wa mwaka huu 2025, yalifanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya THBUB Septemba 22, 2025 Jijini Dar es salaam.