WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA TAALUMA YAO KULINDA HAKI ZA BINADAMU

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa wito kwa waandishi wa habari kote nchini kuzingatia
maadili ya taaluma yao katika kuhabarisha Umma katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu Octoba 2025 ili kulinda haki za binadamu.
Wito huo umetolewa na Makamu mwenyekiti THBUB Mhe. Mohamed Khamis Hamad alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya kwa waandishi wa habari yaliyolenga kuwajengea uwezo kuhusu haki za binadamu na wajibu wa waandishi wa habari.
Mafunzo hayo yamefanyikia katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jijini Arusha Septemba 17, 2025.
Mhe. Hamad wamewakumbusha waandishi wa habari kuwa wana wajibu wa kuripoti habari zao kwa usahihi, kwa uwiano na bila upendeleo kwa chama au mgombea yeyote.
Aidha, amewataka kuepuka matumizi ya lugha ya matusi, kejeli, udhalilishaji, pamoja na kuchapisha au kutangaza taarifa zenye viashiria vya uchochezi, hasa kupitia mitandao ya kijamii.
“Vyombo vya habari ni kiungo muhimu kati ya wananchi, wagombea na taasisi za uchaguzi, hivyo vinapaswa kuwa chanzo cha taarifa sahihi na si chombo cha kueneza taarifa za uongo na potofu. Maadili ya uandishi, uhuru wa habari na ulinzi wa haki za binadamu ni nguzo muhimu zinazopaswa kupewa kipaumbele na kila mwanahabari wakati wa utekelezaji wa majukumu yake amesema Mhe. Hamad.
Aidha, aliongeza kuwa, THBUB inatarajia waandishi wa habari watatekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, hivyo kuchangia uchaguzi wa amani, haki na huru.