WANAWAKE JIJINI DAR ES SALAAM WAOMBA ELIMU ZAIDI KUHUSU HAKI

Wanawake Jijini Dar es salaam wameomba elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora izidi kutolewa katika mikusanyiko ya Wanawake kwani wao mara nyingi wamekuwa wakikosa fursa ya kupata elimu hiyo katika mikutano inayoandaliwa na viongozi wa serikali kutokana na majukumu waliyo nayo.
Rai hiyo imetolewa na wanawake waliotembelea Banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam Julai 9, 2025.
"Tumejifunza mengi leo kuhusu haki zetu kama wanawake, tunaomba elimu hii itufikie katika vikundi vyetu kwani mara nyingi wanawake hushindwa kufika katika mikutano ya vijiji ama mtaa kutokana na shughuli nyingi za nyumbani lakini katika vyama vyetu huwa tunalazimika kwenda kwa kuwa haviwahusu wanaume”.amesema mmoja wa wanawake hao.
Kwa upande wao maafisa wa THBUB wameeleza kuwa Tume inaendelea na juhudi mbalimbali za kuhakisha elimu hiyo inawafikia wananchi katika makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo wanawake kupitia maonesho mbalimbali, warsha, semina na makongamano ili kufikisha ujumbe wa haki za binadamu.
Maafisa hao wameeleza pia kuwa THBUB inatambua changamoto zilizopo katika kufikisha elimu hiyo kwa baadhi ya maeneo lakini inaendelea kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha kuwa elimu ya haki za binadamu inawafikia Watanzania wote bila ubaguzi.