WATOTO WAFUNDISHWA KUKATAA UKATAILI

Katika juhudi za kuimarisha usalama na heshima kwa watoto, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewapatia elimu watoto wa shule ya Msingi Mapambano na Shule ya Sekondari Wailes kuhusu haki zao na kuwataka kutokubali kufanyiwa vitendo vya ukatili kwani vitendo hivyo vinaweza kuleta madhara makubwa kwao.
Elimu hiyo imetolewa na Kamishna wa THBUB, Mhe. Nyanda Shuli alipokuwa akiwafundisha wanafunzi hao waliotembelea banda la Tume katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai 11, 2025.
Mhe. Shuli amewataka wanafunzi hao kutonyamazia vitendo vyote vya kiukatili vinavyofanywa katika jamii dhidi yao ama watu wengine.
“Ukinyamaza wakati haki ya mwenzio inavunjwa na wewe watakaa kimya haki yako itakapovunjwa. Hakuna mtu yoyote atakuchapa ama kupewa adhabu yoyote ukitoa taarifa ya Uvunjwajiwa haki yako ama ya mwenzio” amesema Mhe. Shuli.
Naye Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka THBUB, Bi. Florence Chaki amewafundisha jinsi ya kutambua dalili za unyanyasaji ikiwa ni unyanyasaji wa kimwili, kihisia, kisaikolojia, kingono au kutelekezwa.
Aidha, ameeleza kuwa elimu hiyo itawafanya watoto hao kuelewa haki zao za msingi na kuwafanya kuishi bila hofu, kutambua aina mbalimbali za unyanyasaji na kujifunza jinsi ya kujilinda na kuwajengea uwezo wa kusema “hapana” kwa vitendo visivyofaa kutoka kwa mtu yeyote, ikijumuisha hata wale wanaotokea nyumbani au shuleni.
Akizungumza kwa niaba Shule hizo, Mwalimu Mariana Mbena alisema kuwa wamewaleta Wanafunzi katika Banda la THBUB ili waweze kujua haki zao, wajibu wao kama watoto na waweze kutambua jinsi ya kujilinda. Jambo ambalo litasaidia kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto.