WATUMISHI WA THBUB WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na miongozo ya utumishi wa umma ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa THBUB Bw. Patience Ntwina wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili na uwajibikaji katika utumishi wa umma, pamoja na masuala ya lishe, afya ya akili, na magonjwa sugu yasiyoambukiza mahali pa kazi.
Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 16 Aprili 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Dodoma.
Bw. Ntwina alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa watumishi kwani yanasaidia kukumbushana miongozo ya utendaji kazi na kuimarisha uwezo wa kutoa huduma kwa haki.
"Mafunzo haya ni muhimu katika kuhakikisha utumishi wa umma unazingatia maadili na miongozo husika badala kufuata matakwa yake binafsi," alisema Bw. Ntwina.
Akiwasilisha mada ya Maadili na Uwajibikaji, Bi. Janeth Mishinga, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Maadili katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alieleza kuwa watumishi wanapaswa kuhakikisha huduma wanazotoa zinazingatia sheria, kanuni, taratibu, na viwango bora vya utoaji huduma.
Bi. Janeth aliwataka watumishi kuongeza juhudi katika kujifunza zaidi kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa taasisi za serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati na huduma bora.
Mafunzo haya ya siku moja yanatarajiwa kuongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa THBUB, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora.