ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

Watumishi wa umma waaswa kujituma na kuepuka kufanya kazi kimazoea

15 Apr, 2024
Watumishi wa umma waaswa kujituma na kuepuka kufanya kazi kimazoea
Watumishi wa umma nchini leo Aprili 5, 2024 wameaswa kujituma zaidi, kuwa wakweli, wenye ushirikiano na kujiepusha na kufanya kazi kwa mazoea. Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bwana Gabriel Robi alipokuwa akifunga mafunzo elekezi jijini Dodoma kwa watumishi wapya kutoka THBUB, Uongozi Institute, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Mfuko wa Pembejeo (AGITF). “Kupitia mafunzo haya tunatarajia mtakuwa wa kweli, mtahakikisha mnashirikiana na watumishi wengine katika vituo vyenu vya kazi na mtatenganisha kazi na mazoea ili kuleta ufanisi katika utumishi wa umma,” Bwana Robi alisema. Pia, Kaimu Katibu Mtendaji huyo aliwaonya watumishi hao kuondokana na tabia za kisanii, kujipendekeza kwa viongozi,na kuongea maneno ya uongo. “Hakuna kiongozi atakayevumilia tabia zisizoleta tija katika taasisi,hivyo fanyeni kazi kwa bidii na mkajenge utamaduni unaoimarisha utendaji kazi utakaosaidia kuleta ufanisi kazini,” alisema. Awali Mkurugenzi Msaidizi kutoka THBUB - Utawala, Bibi Portacia Benito alimweleza Mgeni Rasmi kuwa jumla ya Watumishi wapya 15 wamepata mafunzo hayo elekezi pamoja na kufanyiwa upekuzi. Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza kufanyika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) chini ya wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Dar es Salaam yamehitimishwa leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.