WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUIMARISHA UPENDO NA MSHIKAMANO MAHALI PAKAZI

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Jackson Elias Nyamwihula, amewahimiza watumishi wa umma kuendeleza upendo na mshikamano mahali pa kazi ili kuboresha ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Bw. Nyamwihula Ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo elekezi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara Katiba na Sheria Bw. Eliakimu Maswi, kwa watumishi wapya kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Ali Hasan Mwinyi uliopo Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoani Pwani Julai 1, 2025.
Bw. Nyamwihula alieleza kuwa mshikamano kazini si tu huongeza morali ya kazi, bali pia huchochea ubunifu, uwajibikaji, na heshima baina ya wafanyakazi.
"Mahali pa kazi pasipo na upendo na mshikamano ni vigumu kufanikisha malengo ya taasisi. Watumishi wanapaswa kushirikiana, kusaidiana, na kuwa na moyo wa utu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku," alisisitiza Bw. Nyamwihula.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Bi. Marium Kuhanga ambaye ni mhadhiri chuo cha utumishi wa umma amewakumbusha watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili katika utoaji huduma, kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kuheshimu Sheria.
“ Watumishi wa Umma tunapaswa kukumbuka kwamba uadilifu si lazima uwe kazini bali unatakiwa kuwa muadilifu mahali popote kwani chochote utakachofanya cha kuudhi ama kudhalilisha jua kuwa unaathiri taswira ya Serikali na Taasisi yako” Alisema Bi. Marium.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu yameshirikisha jumla ya watumishi 73 ambapo watumishi 39 ni kutoa THBUB.