ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

Watumishi wa umma watakiwa kujua majukumu ya taasisi zao

15 Apr, 2024
Watumishi wa umma watakiwa kujua majukumu ya taasisi zao
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bwana Gabriel Robi amewataka watumishi wapya katika utumishi wa umma nchinikuyajua vyema majukumu ya taasisi zao na kutoa huduma bora kwa wananchi. Pia, amewataka watumishi hao kuwa na ushirikiano kazini, kutunza siri za ofisi, kuwa wavumilivu, na kuushirikisha uongozi pindi wapatapo changamoto mbalimbali. Bwana Robi ameyasema hayo leo Aprili 3, 2024 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya kutoka THBUB,Uongozi Institute,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Mfuko wa Pembejeo (AGITF), yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) jijini Dodoma. “Baadhi ya watumishi wanayafahamu majukumu ya idara zao tu, lakini ufahamu wao ni mdogo juu ya majukumu ya taasisi;hili halikubaliki,” Kaimu Katibu Mtendaji huyo alisema, na kuongeza kuwa “ni wajibu wa kila mtumishi kujua majukumu ya taasisi yake.” Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka THBUB anayeshughulika masuala ya Utawala, Bibi Portacia Benito alimshukuru Bwana Robi kwa nasaha zake nzuri kwa watumishi wapya na kwa kufungua mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya siku tatu yanaendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Dar es Salaam na yanatarajia kuongeza uwajibikaji mahala pa kazi, uzingatiwaji wa sheria, taratibu za kazi, na kuleta tija na ufanisi katika utendaji kazi. Jumla ya watumishi wapya 16, kati yao 10kutoka Ofisi kuu ya THBUBjijini Dodoma watanufaika na mafunzo hayo, ambapo mada mbalimbali, zikiwemo: Muundo wa Serikali na uendeshaji wake, Kanuni za utumishi wa umma, huduma bora kwa mteja na nyinginezo zitatolewa.