WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUENDELEA KUIWEZESHA THBUB

Waziri wa Katiba na Sheria, Dr. Damas Ndumbaro amesema kuwa Wizara itaendelea kuiwezesha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Dr. Ndumbaro ameyasema hayo alipotembelea banda la THBUB katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Julai 11, 2025.
“Hongereni kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha umma, Wizara inatambua mchango wenu katika maswala ya haki na misingi ya utawala bora. Hivyo tutahakikisha kwamba tunaendelea kuwawezesha kifedha ili muendelee kuifanya kazi ya kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa”.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeendelea kushiriki maonesho hayo yenye kaulimbiu "Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania", kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora, kusikiliza na kutatua malalamiko ya uvunjaji wa haki na kutoa ushauri wa kisheria bure.