MPELUMBE AKABIDHIWA OFISI RASMI
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe amekabidhiwa Ofisi rasmi na mtangulizi wake Mhe. Jaji (mst.) Mathew P. M. Mwaimu katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za Tume, Mtaa wa Makole Jijini Dodoma na kushuhudiwa na Katibu Mtendaji, Bw. Patience Ntwina leo Novemba 04, 2026.
Mhe. Mwaimu, ambaye aliongoza Tume hiyo kuanzia mwaka 2019 hadi 2026, amemkabidhi ofisi Mhe. Mpelumbe aliyeteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Jaji ( Mst) Mwaimu ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano na ushauri walioutoa, uliowezesha Tume kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea haki za binadamu pamoja na kusimamia misingi ya utawala bora nchini.
Aidha, ameitoa wito kwa uongozi mpya wa THBUB kuendeleza na kukamilisha miradi aliyoiacha, ikiwemo kifuatilia uhuishaji wa Mpangokazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu, kufuatilia kuhuisha Awamu ya Pili ya Mpangokazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na kukamilisha nyenzo/ mwongozo wa tathmini ya misingi ya utawala bora nchini.
Mhe. Jaji (Mst) Mwaimu pia amemshukuru Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwa. Patience Ntwina, Naibu Katibu Mtendaji, Bwa. Juma Msafiri Karibona, Menejimenti na watumishi Tume kwa ushirikiano waliompatia yeye na Makamishna waliomaliza muda wao wa uongozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa THBUB, Mhe. Wakili Mpelumbe, ameupongeza uongozi uliomaliza muda wake kwa weledi, uadilifu, utumishi uliotukuka na mchango wake katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Tume.
Mhe. Wakili Mpelumbe ameahidi kuendeleza kazi zilizoanzishwa na uongozi uliomaliza muda wake huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Tume.
“Mmesimamia mambo muhimu na kushauri mambo mengi ya kiserikali na kimataifa. Tunawashukuru sana na tunawapongeza kwa utumishi uliotukuka, kwa kutekeleza majukumu kwa weledi na uaminifu wa hali ya juu,” amesema Mhe. Wakili Mpelumbe.
Vilevile, Mhe. Wakili Mpelumbe ameomba kuendelea kupata ushirikiano na ushauri kutoka kwa Mhe. Mwaimu na Makamishna waliomaliza muda wao, akibainisha kuwa uzoefu wao ni muhimu katika kuimarisha utendaji wa Tume na kuendeleza juhudi za kulinda haki za binadamu na kusimamia utawala bora nchini.

