MPELUMBE AMEAHIDI UONGOZI WA WELEDI NA HAKI BILA UPENDELEO
Mwenyekiti mpya wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Dunford George Mpelumbe, ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi, ufanisi, uadilifu na bila upendeleo, akisisitiza kuwa kipaumbele cha uongozi wake ni kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na misingi ya utawala bora inazingatiwa.
Mhe. Mpelumbe ameyasema hayo alipokutana kwa mara ya kwanza na kuzungumza na watumishi wa THBUB katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Makao Makuu ya Tume, zilizopo katika Jengo la PSSSF, Mtaa wa Makole, jijini Dodoma, baada ya kuapishwa kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Novemba 2, 2026.
Amesema yeye pamoja na Makamu Mwenyekiti wamejipanga kuhakikisha Tume inatekeleza ipasavyo dhamana yake ya kikatiba ya kulinda haki za binadamu na kusimamia misingi ya utawala bora bila kuathiriwa na upendeleo wa aina yoyote.
"Tumejipanga kutekeleza majukumu yetu kwa weledi wa hali ya juu na bila upendeleo wa namna yoyote. Dhamana yetu mimi na Makamu Mwenyekiti ni kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa na misingi ya utawala bora inazingatiwa," amesema Mhe. Mpelumbe.
Aidha, amesema katika kipindi cha uongozi wake, THBUB itaandaa Mpango Mkakati utakaozingatia mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba katika kulinda haki za binadamu na kusimamia utawala bora nchini.
Akizungumzia ushirikiano kati ya Tume na Serikali, Mhe. Mpelumbe amesema anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa THBUB kutekeleza majukumu yake. Ameeleza kuwa uongozi mpya utaendeleza mazuri yaliyofanywa na viongozi waliotangulia, huku ukitekeleza maelekezo ya Mhe. Rais na kuimarisha wajibu wa Tume kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata na kunufaika na haki zinazotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Akitoa matarajio yake kwa watumishi wa Tume, Mhe. Mpelumbe amewataka kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, ushirikiano na utendaji unaozingatia matokeo, akisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutimiza wajibu wake kwa weledi na kujituma.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Tume yanategemea kwa kiasi kikubwa mshikamano na uwajibikaji wa watumishi wake, hivyo amewahimiza kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Tume

