emblem

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu

Habari

THBUB na TLS wafungua ukurasa mpya wa ushirikiano


Na Germanus Joseph MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mst.) na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dkt. Edward Hosea wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili na kuwa na programu nyingi zaidi za pamoja. Hayo yamebainishwa leo (Mei 4, 2021) katika mazungumzo baina ya viongozi wa taasisi hizo mbili yaliyofanyika makao makuu ya ofisi za Tume, mtaa wa Kilimani jijini Dodoma. Kimsingi THBUB na TLS wamekubaliana kuongeza wigo wa maeneo ya ushirikiano waliyokuwanayo awali kwa kuingiza masuala mengi zaidi ya kushirikiana. Kwa mujibu wa mazungumzo yao taasisi hizo zinatafakari kuwa na programu za pamoja zinazolenga kukomesha uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ngazi ya vijiji na tarafa, kupunguza msongamano magerezani na kuimarisha utawala wa sheria nchini. Pia taasisi hizo zinatafakari kuwa na mashirikiano katika ngazi za mikoa na kanda kupitia ofisi za TLS zilizofunguliwa hivi karibuni katika maeneo hayo. “Sisi Mheshimiwa President nakuhakikishia tuko tayari kufanyakazi na nyinyi, lakini tukiamini kwamba tutafanyakazi katika namna ya kusaidia zaidi kuliko kuharibu,” Mhe. Mwenyekiti wa THBUB alimwambia Dkt. Hosea na ujumbe wake. Mhe. Mwaimu alisema kuwa anaamini maeneo ya ushirikiano yaliyobainishwa endepo yatafanyiwa kazi vizuri yanaweza kuisaidia Serikali na wananchi kwa ujumla. Mwenyekiti wa Tume alitumia fursa hiyo pia kuueleza ujumbe wa TLS majukumu ya Tume, na kwamba taasisi hiyo inatumia zaidi njia ya mazungumzo katika utatuzi wa migogoro na uwasilishaji wa mapendekezo yake kwenye mamlaka husika na kwamba njia hiyo imekuwa na mafanikio makubwa. Aidha, Kiongozi huyo aliishauri TLS kutojihusisha na masuala ya kisiasa, kutoegemea upande wowote katika utendaji wao, kuwa wazalendo na kuwa mabalozi wazuri wa Tume. Mwisho, Mhe. Mwaimu aliipongeza TLS kwa kuendesha vizuri zoezi la uchaguzi wa viongozi uliofanyika ndani ya taasisi hiyo hivi karibuni na safu ya uongozi mpya kuwa na mchanganyiko wa vijana na wazee. Pia aliipongeza na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuitembelea Tume. Kwa upande wake, Dkt. Hosea alimweleza Mhe. Mwaimu na timu yake kuwa taasisi yake ingependa kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na Tume kwa kuwa na programu za pamoja kwa vile malengo ya taasisi hizo mbili yanashabihiana kwa kiwango kikubwa. Alisema anatambua kuwa TLS na THBUB walitiliana saini makubaliano ya ushirikiano (MoU) kuhusu utoaji wa machapisho mawili yaitwayo “Haki na Usalama” na “Ulinzi na Usalama,” lakini ipo haja ya kuongeza ushirikiano zaidi. “Nadhani ni wakati sasa wa kuipitia tena hiyo MoU tuone tunaipanua vipi tuweze kuwa na mashirikiano mapana zaidi,” Dkt. Hosea alisema. Rais huyo wa TLS aliipongeza Tume kwa namna inavyofanyakazi licha ya changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo na aliushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa mapokezi na mazungumzo mazuri waliyoyafanya.